Mageuzi ndiyo dawa pekee ya kuiponya IEBC – Akombe

Na RUTH MBULA

KAMISHNA wa zamani wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ametaka tume hiyo ifanyiwe mageuzi sasa ili kuepuka vurugu zinazotokana na madai ya wizi wa kura.

Dkt Roselyn Akombe aliyekuwa akizungumza katika hafla iliyoandaliwa na vuguvugu la Diaspora Must Vote (KDMV) jimboni Minnesota, Amerika, alisema kuwa uchaguzi wa 2022 hautakuwa huru na wa haki iwapo tume ya IEBC haitafanyiwa marekebisho sasa.

Dkt Akombe pia alitetea IEBC kuhusu madai kwamba tume hiyo ndiyo iliyochelewesha kutekelezwa kwa sheria inayotaka Wakenya wote wanaoishi ughaibuni kupiga kura.

Dkt Akombe alisema wanasiasa kutoka upinzani na serikalini ndio wanaostahili kulaumiwa kwa kuchelewesha utelekezaji wa sheria hiyo. Dkt Akombe alidai kuwa wanasiasa hawataki Wakenya wanaoishi ughaibuni kushirikishwa katika uchaguzi.

“Mageuzi katika tume ya IEBC ni muhimu katika kuhakikisha kuwa uchaguzi wa 2022 unakuwa huru na wa haki,” akasema Dkt Akombe. Dkt Akombe alisema kuwa chama tawala cha Jubilee na wanasiasa wa Upinzani wamesalia kimya kuhusu mageuzi ndani ya IEBC huku muda ukizidi kuyoyoma.

“Inaonekana wanasiasa kutoka upande wa serikali wanataka kuendelea na tume iliyopo sasa kwa sababu wanadhani itawafaa wao 2022,” akasema Dkt Akombe.

Kamishna huyo wa zamani wa IEBC alilitaka vuguvugu kushinikiza kufanyika kwa mabadiliko ndani ya IEBC badala ya kungojea uchaguzi utakapokaribia.

Dkt Akombe, hata hivyo, alisema ana matumaini kwamba siku moja Kenya itakuwa na uchaguzi huru na haki kama ulioshuhudiwa 2002.

“Kabla ya kuwa na uchaguzi huru na wa haki kuna haja ya Wakenya kushinikiza mageuzi ndani ya tume ya IEBC,” akaongezea.

Habari zinazohusiana na hii

Ruto aitetea IEBC

IEBC yaanika uozo wake