Uozo katika hospitali nne za rufaa unavyolemaza utoaji huduma
Na CHARLES WASONGA
HOSPITALI nne za rufaa humu nchini zimezongwa na matatizo kiasi kwamba utoaji wa huduma zisizoafiki viwango vya kimataifa, ripoti iliyowasilishwa bungeni juzi imethibitisha.
Hali katika hospitali hizi ni taswria ya namna sekta ya afya, ambayo sasa imegatuliwa, imesambaratika kutokana na ukosefu wa vifaa muhimu na wahudumu wa kutosha.
Ripoti iliyotolewa na Kamati ya Bunge kuhusu Afya inafichua kuwa huenda shughuli katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH), Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Moi (MTRH), Hospitali ya Kitaifa ya Kutibu Magonjwa ya Uti wa Mgongo (National Spinal Injury Hospital) na Hospitali ya Kitaifa ya Mafunzo na Rufaa ya Mathari zikakwama kwa sababu zinazongwa na madeni, ukosefu wa vifaa na wahudumu wasiohitimu.
Baadhi ya paa za majengo katika hospitali hizo zinavuja, kuta zimechina kwa kutopakwa rangi kwa muda mrefu ilhali huko ndiko maelfu ya Wakenya wenye mapato ya chini hukimbilia kutafuta huduma za afya.
Na mara nyingi wao hupewa huduma duni au kukosa kuhudumiwa. Na vifaa, ikiwa vipo, huwa ni kuu kuu kiasi kwamba haviwezi kutumika kwani huwa vimerundikwa kwenye stoo zenye vumbi.
Kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge Mwakilishi wa Murang’a, inasema hali hiyo inachangiwa na kupunguzwa kwa bajeti za hospitali, matatizo ya kifedha na ufadhili finyu kila mara kutoka kwa serikali na mashirika fadhili tangu taifa hili lilipopata uhuru.
“Hili ni tatizo sio tu katika hospitali za rufaa bali katika hospitali nyingi za umma humu nchini,” kamati hiyo ikasema.
“Hospitali ya KNH ambayo ndio hospitali kubwa na ya zamani ya rufaa nchini na Afrika Mashariki inazongwa na matatizo kutokana na ufadhili finyu kila mwaka haswa kutoka kwa Hazina ya Kitaifa,” ripoti hiyo inaeleza.
Wakati huu, kamati hiyo inakadiria kuwa KNH inahitaji jumla ya Sh8 bilioni kwa mwaka ili iweze kutoa huduma ipasavyo. Kando na hayo, inakabiliwa na tatizo la wagonjwa kufeli kulipa bili zao hali inayopelekea wao kuzuiliwa hospitalini humo kwa muda mrefu.
“Aidha, hospitali hiyo inakumbwa na uhaba mkubwa wa wafanyakazi kwani wafanyakazi 1,456 walioko sasa hawatoshi. Inahitaji wafanyakazi 3,000 ili iweze kutoa huduma ipasavyo,” ikasema ripoti hiyo iliyowasilishwa bungeni na Bi Chege.
Kando na hayo, hospitali hiyo pia inakabiliwa na tatizo la usimamizi baada ya mahakama kusitisha mchakato wa uajiri wa Afisa Mkuu Mtendaji mpya kuchukua mahala pa Lily Koros aliyefutwa kazi mwaka jana.
Hospitali ya Mathari, kwa upande wake pia inazongwa na tatizo la uhaba wa wafanyakazi wa viwango vyote, hali ambayo imeathiri utoaji huduma.
Kwa mfano, mwezi jana wabunge wanachama wa kamati hiyo ya Afya walipozuru hospitali hiyo walipata kwamba muuguzi mmoja alikuwa akiwahudumia wagonjwa 147.
Ripoti hiyo pia anaelezea hofu kuhusu hali mbaya ya majengo katika hospitali hiyo ambayo ni kuukuu, kuta zina mashimo nap aa zinavuja.
“Kando na hayo hospitali hiyo pia inakosa vifaa vya kimsingi na miundo mbinu kama vyoo, bafu, mitaro ya kuondoa maji taka,” ripoti hiyo inasema.
Kitengo cha ulinzi mkali, ambacho huhudumia wagonjwa walioletwa hapo na mahakama, pia kinakumbwa na msongamano kwa sababu wagonjwa hukaa kwa muda mrefu. Hii ni kwa sababu amri ya mahakama inahitajika kabla ya wagonjwa hao kuruhusiwa kuondoka.
“Shida kuu ni ya kifedha. Sababu ni kwamba wagonjwa ambao hupelekwa huko na mahakama ili kukaguliwa hali yao ya kiakili kubaini ikiwa wanaweza kujibu mashtaka huwa hawalipiwi baada ya huduma hizo kutolewa,” ikasema ripoti hiyo.
Na katika Spinal Injury Hospital, kamati hiyo inasema, inakabiliwa na changamoto ya vifaa na wafanyakazi kwani hupokea wagonjwa kutoka hospitali za humu nchini na zile za Afrika Mashariki na Kati.
“Na wafanyakazi wachache walioko hawana ari na msukumo wa kufanyakazi kwa bidii kwa sababu wengine wamesalia katika daraja moja la kazi kwa miaka mingi bila kupandishwa vyeo,” ripoti hiyo inaeleza.
Sawa na hospitali zingine za rufaa, hospitali hii pia inakabiliwa uhaba wa vifaa vya kimatibabu kama vile vitanda maalum (orthopaedic beds), mashine za maabara, ‘spinal opereshen sets” na vile vya kutumiwa katika vitengo vya kuwahudumia wagonjwa mahututi (ICU), kati ya vingine.
Hospitali ya MTRH nayo licha ya kuhudumia watu 25 milioni kutoka kaunti 21 za Rift Valley na Magharibi mwa Kenya inakabiliwa na changamoto ya kifedha, mzigo wa madeni na ukosefu wa wahudumu wa kutosha.
Na kufikia Januari 31 mwaka huu hospitali hiyo ilikuwa ikadai Sh313.8 milioni kutoka kwa kampuni mbalimbali na Sh514.6 milioni kutoka watu binafsi.