MAPISHI: Chipsi na kuku
Na MARGARET MAINA
IKIWA makazi yako ni mjini au shughuli zako za kujiingizia kipato ni za mjini bila shaka unatambua jinsi ambavyo viazi vilivyokatwa vipande vidogovidogo na kukaangwa kwa mafuta – yaani ribendo – vimepata umaarufu mkubwa.
Hiki ndicho chakula kinachonunuliwa zaidi kwa watu wasio na muda wa kupoteza.
Muda wa kuandaa: Dakika 15
Muda wa kupika: Nusu saa
Walaji: 3
Vinavyohitajika
- Kuku ½ kilo
- Viazi ulaya ½ kilo
- Nyanya 2
- Kitunguu saumu ¼ kijiko
- Tangawizi ¼ kijiko
- Majani ya giligilani ¼ kijiko
- Chumvi ½ kijiko
- Pilipili manga kijiko 1
- Mafuta ya kupikia
- Apple cider vinegar ½ kikombe
- Kitunguu maji 1
Maelekezo
Menya viazi kisha kata viwe vipande virefu lakini vyembamba kabisa kiasi cha chipsi unazopenda.
Hifadhi vizuri kwenye maji yaliyotiwa chumvi.
Safisha kuku vizuri kisha weka kwenye sufuria safi. Mimina vinegar juu ya kuku. Bandika sufuria ya kuku jikoni. Acha ichemke vizuri. Kisha toa.
Weka kikaangio motoni kisha tia mafuta ya kupikia. Mafuta yakipata moto, weka viazi na kaanga hadi chipsi ziive. Epua na hifadhi pembeni. Rudia hadi viazi vyote viwe vimeiva.
Kaanga kuku kwenye mafuta uliyotumia kupikia chipsi.
Bandika sufuria mekoni kisha weka mafuta. Yakipata moto, tia kitungu maji na viungo vyote ila usiweke nyanya.
Vitunguu vikianza kubadilika rangi ndipo unapaswa kuongeza nyanya. Nyanya zikiwa tayari zimehaiva, weka kuku na funika vizuri kwa dakika tano.
Ongeza supu ya kuku nusu kikombe kwenye sufuria kisha acha ichemke.
Weka chipsi kwenye sufuria yenye sauce ya kuku na pika hadi supu ikaukie.
Epua, kisha pakua na ufurahie mlo wako.