Kamari ya urais ya Ndidi Nyoro akikaidi Gachagua mlimani
Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro amejipata katikati ya vita vya kisiasa katika Mlima Kenya tangu alipotangaza azma ya kuwania urais, akipuuza chama cha UDA na kujiunga na People’s Party of Kenya (PPK).
Mbunge huyo anayehudumu muhula wa pili amekuwa akishambuliwa na washirika wa aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, ambao wanadai ni kibaraka wa serikali ndani ya upinzani, anayetaka kugawanya kura za eneo la Mlima Kenya.
Lakini Nyoro anasema hana mpango wa kugawanya eneo hilo na yuko tayari kumuunga mkono mgombea yeyote atakayechaguliwa na upinzani kwa makubaliano.
Katika mahojiano maalumu na Taifa Leo , alisema alijiunga na upinzani akiwa na ajenda ya kubadilisha nchi, wala si kwa mwaliko wa kiongozi yeyote.
“Ikiwa ni Gachagua, nitamuunga mkono. Wakinichagua mimi, ninatumai naye ataniunga mkono. Kwa hivyo, ni kura gani ninazogawanya?” aliuliza.
Alikanusha pia madai kuwa PPK ni mradi wa kumsaidia Rais William Ruto kugawanya kura za Mlima Kenya, akisema chama hicho kilianzishwa mwaka 1996, kabla ya Jubilee na DCP.
Alisema alichukua usimamizi wa chama hicho mwaka 2024 na kujiunga rasmi miezi miwili iliyopita ili kupata nafasi ya kutekeleza ajenda yake bila kutegemea maamuzi ya viongozi wengine.
Nyoro, ambaye zamani alikuwa mshirika wa karibu wa Rais Ruto, alisema uhusiano wao ulianza kuzorota wakati wa mchakato wa kumuondoa Gachagua mamlakani mwaka 2024.
Alisema kutoshiriki kwake katika mchakato huo kulimfanya kuwa adui wa Rais, na baadaye akavuliwa uenyekiti wa Kamati ya Bajeti ya Bunge la Kitaifa.
Alikanusha madai ya kupokea Sh30 milioni ili kukosa kikao cha kumuondoa Gachagua mamlakani, akisema hahitaji kuhongwa ili kufanya maamuzi ya kisiasa.
Pia alimtaka Seneta wa Nyandarua John Methu kuthibitisha madai hayo, akidai kuwa yeye mwenyewe alimsaidia kifedha wakati wa uchaguzi mdogo wa Ol Kalou.
Licha ya mzozo huo, Nyoro alisema bado ana uhusiano mzuri na Gavana wa Murang’a Irungu Kang’ata, akisisitiza kuwa tofauti za kisiasa hazipaswi kugeuzwa uhasama wa kibinafsi.
Kuhusu uhusiano wake na kiongozi wa Jubilee Fred Matiang’i, alisema mazungumzo yao yanalenga mustakabali wa nchi, wala si kugawana mamlaka.
Alisema yuko tayari kufanya kampeni pamoja na Gachagua, Kalonzo Musyoka au kiongozi mwingine yeyote wa upinzani, lakini hatakubali kulazimishwa kumfuata mtu.
“Asiyetaka kufanya kazi nami, ni uamuzi wake,” alisema.
Nyoro anasema azma yake ya kuwania urais haikutokana na msukumo wa ghafla. Alisema amekuwa akijiandaa kwa muda kwa kujifunza kuhusu changamoto za nchi na kujiendeleza kitaaluma.
Mbunge huyo ana shahada za uzamili katika uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi na Chuo Kikuu cha Kenyatta, na amehudhuria kozi za uchumi na maendeleo katika London School of Economics. Pia alisema alihitimu na cheti cha juu cha uchumi wa maendeleo kutoka Chuo Kikuu cha Harvard Aprili mwaka huu.
Alisema uongozi mzuri unahitaji nia njema pamoja na uwezo wa kutekeleza majukumu.
Mbali na siasa, Nyoro amekuwa akijenga jina katika biashara na uwekezaji. Alisema alianza kujifunza kuhusu soko la hisa akiwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kenyatta.
Alisema alianza kununua hisa za Kenya Power kuelekea uchaguzi wa 2017, wakati hisa moja ilikuwa ikiuzwa kwa Sh1.50 na kampuni hiyo ikipata hasara.
Alitumia takriban Sh46 milioni kununua hisa hizo hatua kwa hatua. Kwa sasa, alisema anamiliki hisa milioni 27 kupitia jina lake na kampuni zake mbili, Limpopo Capital na Sahara, za thamani ya takriban Sh594 milioni kwa bei ya Sh22 kwa hisa.
Alikanusha madai kuwa anashikilia hisa hizo kwa niaba ya Rais Ruto, akisema uwekezaji wake ulianza kabla hajawa mbunge.
Nyoro pia alitetea rekodi yake ya kusimamia hazina ya maendeleo ya maeneo bunge (CDF) Kiharu, akisema siri ni kutumia wafanyakazi wa eneo husika badala ya wakandarasi wakubwa.
Alisema mfumo huo umesaidia kuboresha shule zote 120 za msingi za umma, huku taasisi 70 zikiwa na sakafu za cabro. Shule nyingine 20 zinatarajiwa kunufaika Desemba.
Kupitia mpango wa Kiharu Masomo Bora, wanafunzi 12,000 katika shule za upili za kutwa 65 hupata chakula kwa kuchangia Sh500 kila muhula. Mpango huo pia unawapa chakula wanafunzi wanaohudhuria masomo ya ziada Jumamosi.
Hata hivyo, Nyoro alisema changamoto kubwa ya uchumi wa Kenya ni deni la taifa, akidai Sh80 kati ya kila Sh100 za matumizi ya serikali huenda kulipa madeni. Alionya kuwa hali inaweza kuwa mbaya zaidi kabla ya Rais Ruto kuondoka mamlakani.
Pia alikosoa kile alichokiita mfumo wa upendeleo katika biashara, ambapo viongozi hutumia mamlaka yao kujinufaisha katika sekta mbalimbali.
Licha ya kujitetea dhidi ya tuhuma za kuwa kibaraka wa serikali, Nyoro anakabiliwa na mtihani wa kuwashawishi wapinzani kuwa azma yake ya urais inalenga kuimarisha upinzani, si kuudhoofisha.
Anasema lengo lake ni upinzani kupata mgombea mmoja wa urais kupitia makubaliano ya haki na ya wazi, na yuko tayari kumuunga mkono atakayechaguliwa, iwapo hatakuwa yeye.