• Nairobi
  • Last Updated April 16th, 2024 12:47 PM
Wakazi wa Thika wahimizwa kupanda miti kuhifadhi mazingira

Wakazi wa Thika wahimizwa kupanda miti kuhifadhi mazingira

Na LAWRENCE ONGARO

KUNA haja ya kupanda miti kila sehemu nchini ili kuhifadhi mazingira ambayo yanaonekana kupoteza mvuto kutokana na ukame ambao umeshuhudiwa miezi kadhaa ambayo imepita.

Mhandisi wa kampuni ya maji ya mjini Thika (Thiwasco) Mhandisi Moses Kinya alisema mnamo wikendi kwamba upanzi wa miti katika kila sehemu nchini unastahili kutiliwa maanani kwa minajili ya kuhifadhi mazingira.

Mkurugenzi wa kampuni ya maji ya Thika (Thiwasco) Mhandisi Moses Kinya (aliye na kilemba) ahutubia waandishi wa habari wakati wa upanzI wa miti eneo la Ngoingwa mwishoni mwa wiki jana. Picha/ Lawrence Ongaro

“Tutafanya juhudi kuona ya kwamba shughuli ya upanzi wa miti inaendeshwa kila mara ambapo tutahimiza kuwa unapokata mti moja ni sharti upande mitano. Tukifanya hivyo, bila shaka mazingira yataimarika pakubwa hapa nchini,” alisema Bw Kinya.

Alisema miti yote inayopandwa ni sharti ipewe maji ama kwa unyunyuziaji ili iweze kunawiri.

“Upanzi wa miti unafaa uwe ni jukumu la kila mmoja wetu. Tusiweke kazi hiyo kuwa ni kazi ya watu fulani,” alisema Bw Kinya.

Miti 5,000

Aliyasema hayo mnamo Jumamosi eneo la Ngoingwa, Thika wakati wa shughuli ya upanzi wa miti ambapo miti 5,000 ilipandwa.

Wakati wa shughuli hiyo, shule ya upili ya Mary Hill, na ya msingi ya Kisiwa zilijumuika pamoja na wafanyakazi wa maji wa Thiwasco na wakazi wa Ngoingwa kupanda miti.

Alisema yeye kama mkurugenzi wa kampuni ya maji ya Thiwasco atafanya juhudi kuona ya kwamba wakazi wa Thika na vitongoji vyake wanapata maji kwa wingi.

Alisema tayari wanapanga kujenga kituo cha kuhifadhi maji eneo la Mary Hill ambapo gharama yake itafikia takribani Sh900 milioni.

“Iwapo kituo hicho kitakamilika, bila shaka kitatoa maji mengi yatakayotoshea wakazi wa Thika na vitongoji vyake kwa jumla.

Mwenyekiti wa bodi ya maji ya kampuni hiyo ya maji, Mhandisi Joseph Kimani, alisema ni muhimu kwa kila mmoja kujihusisha na upanzi wa miti  ili kulinda mazingira.

“Ili kufanikisha shughuli hii ni sharti washikadau na wahusika wote wahusishwe. Shughuli hii haipaswi kuachwa kwa watu fulani bali ni kazi ya kila mmoja wetu,” alisema Bw Kimani.

Diwani wa eneo hilo Bw Andrew Kmani alisema yeye kama kiongozi wa eneo hilo atahakikisha kila wakati miti inapandwa ili kuhifadhi mazingira  kikamilifu.

“Sisi wote tunastahili kujihusisha na upanzi wa miti. Na iwapo tutafanya hivyo, bila shaka tutapiga hatua kubwa,” alisema Bw Kimani.

Aliwaomba viongozi wengine na washikadau wote waache kusikiza siasa na badala yake wajihusishe na maendeleo ambayo Rais Uhuru Kenyatta anahimiza kila mara.

“Mimi kwa upande wangu sitaki kujihusisha na siasa lakini ajenda yangu kuu ni kuona nimetekeleza wajibu wangu kama kiongozi na kutumikia wananchi wote bila kubagua yeyote,” alisema Bw Kimani.

You can share this post!

ULIMBWENDE: Makosa ambayo baadhi ya watu hufanya wakati wa...

AFYA NA ULIMBWENDE: Vyakula vitakavyokuza nywele zako

adminleo