Hatimaye Uhuru apatikana baada ya wiki mbili
Na BENSON MATHEKA
HATIMAYE, Rais Uhuru Kenyatta alionekana hadharani Jumatatu baada ya kutoonekana ama kusikika kwa wiki mbili.
Kulingana na Msemaji wa Rais, Bi Kanze Dena, Rais Kenyatta amekuwa ofisini mwake katika Ikulu ya Nairobi akichapa kazi na kufikiri kwa undani kwa wiki hizo mbili
“Huwa ninashangaa watu wanaposema kwamba Rais ametoweka. Rais Kenyatta amekuwa katika ofisi yake akishughulikia masuala kadhaa na pia akitafakari. Rais yuko salama, mwenye afya na mchangamfu kama kawaida yake,” alisema Bi Dena.
Baadaye jana, Bi Dena alituma taarifa na picha za kuonyesha Rais Kenyatta akitia sahihi miswada kadhaa kuwa sheria na kukutana na ujumbe kutoka Marekani.
Rais Kenyatta alionekana hadharani mara ya mwisho alipotoka China wiki mbili zilizopita kwenye ziara aliyoandamana na kinara wa ODM, Raila Odinga.
Tangu wakati huo, hakuwa akihudhuria hafla yoyote, kutoa taarifa ama hata kuonekana kwenye picha.
Kusokena huko kwa rais hadharani kulizua uvumi miongoni mwa Wakenya hasa wanaotumia mitandao ya kijamii wakitaka kujua aliko.
Jana, Bi Dena alitetea kukosekana kwa rais hadharani akisema amekuwa akifanya kazi ofisini mwake kwa wiki hizo mbili. Kulingana naye, sio lazima Rais aonekane hadharani ili ijulikane yuko salama na kuwa anafanya kazi.
Akizungumza na kituo kimoja cha redio jana asubuhi, Bi Dena alisema tofauti na marais wengine ambao huwa wanaangaziwa kila wakati kwenye vyombo vya habari, Rais Kenyatta anahitaji muda wa kutafakari na kufanya maamuzi kuhusu nchi.
Uvumi kuhusu Rais Kenyatta kutoweka hadharani zilichangiwa na kufungwa kwa anwani za mitandao ya kijamii za Rais Kenyatta mnamo Machi 22. Tangu wakati huo, Wakenya wamekuwa wakitegemea mawasiliano kutoka kwa Bi Dena.
Kupitia Twitter, Bi Dena alisema kwamba anwani za mitandao ya kijamii za Rais Uhuru Kenyatta ni zake za kibinafsi na ana haki ya kuzifunga na kuzifungua akitaka.
Rais Kenyatta amekuwa na kipindi kigumu kisiasa na kusimamia nchi kutokana na kutengwa na wanasiasa wa Jubilee hasa kutoka ngome yake ya Mlima Kenya. Baadhi wanamlaumu kwa madai ya “kumsaliti” Naibu Rais William Ruto kuhusu uchaguzi wa 2022. Wengine nao wanasema amepuuza eneo hilo kimaendeleo na kunao wanaolalamikia mwafaka wake na kiongozi wa ODM, Raila Odinga.
Katika uongozi wa nchi, Rais Kenyatta anakabiliwa na hatari ya kushindwa kutimiza Nguzo Nne Kuu, gharama ya maisha imepanda, uhaba wa kazi, kuyumba kwa sekta ya kilimo miongoni mwa matatizo mengine tele yanayowakumba wananchi wa kawaida.
Vita dhidi ya ufisadi navyo vimeonekana kufifia huku baadhi ya mawaziri na maafisa wengine wa ngazi za juu wakiendelea kuwa serikalini wanapochunguzwa kwa madai ya ufisadi.