• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 3:03 PM
Lusaka na Murkomen ni wasaliti – Maseneta

Lusaka na Murkomen ni wasaliti – Maseneta

Na PETER MBURU

MASENETA Jumanne waliwakaanga Spika wa Seneti Ken Lusaka na kiongozi wa wengi Seneti Kipchumba Murkomen, kwa uwepo wao katika afisi ya Rais alipokuwa akitia sahihi mswada wa marekebisho kwenye sheria ya afya, ambao haukupitishwa na bunge hilo.

Maseneta hao walitaja hatua ya Bw Lusaka na Bw Murkomen kuwa usaliti, wakisema hata baada ya Bunge la Seneti kudharauliwa kwa sheria hiyo kurukishwa bila kupitishiwa huko, wawili hao bado walienda kuwa na Rais alipokuwa akitia sahihi kwenye mswada huo.

Walilalamika kuwa kumekuwa na mazoea ya sheria ambazo zinapitishwa katika Bunge la Kitaifa kurukishwa bila kupitishiwa seneti, wakiapa kuwa watafika katika Mahakama ya Juu zaidi Nchini ‘kuomba ushauri’.

“Tumekuwa tukidharauliwa na hivyo sasa suluhu ni twende katika Mahakama ya Juu zaidi Kenya iamue kuhusu suala hili mara moja. Tuorodheshe sheria zote ambazo zimepitishwa bila mchango wa seneti na tuiombe mahakama kuzitaja kuwa kinyume na sheria,” akasema seneta wa Siaya James Orengo.

Seneta Murkomen alijaribu kujitetea kuwa hakuwa na habari kuwa mswada kuhusu marekebisho kwenye sheria ya afya ulifaa kutiwa sahihi, akisema kuwa alitarajia ule wa seneta wa Kiambu kuhusu kuingia mamlakani kwa magavana wapya pekee.

Lakini maseneta walikuwa na ghadhabu, wakisema wamekuwa wakilalamika kuwa wanadharauliwa na Bunge la Taifa, ilhali uongozi wao pia unaendeleza dharau hizo kwa kuhudhuria tukio hilo licha ya kuwa sheria haikuwa imefuatwa.

“Sisi wenyewe tunajiweka chini na tunazidi kudharauliwa kwa matukio kama haya,’ akasema seneta wa Homa Bay Moses Kajwang.

“Spika Lusaka na Bw Murkomen walikuwa hapo na tunabaki tukishangaa sasa sisi tufanye nini,” akasema seneta wa Kisii Sam Ongeri.

Ni hapo ambapo maseneta waliamua kufika kortini kutafuta suluhu ya mgogoro baina yao na wabunge.

You can share this post!

MKASA WA SOLAI: Siasa zachelewesha fidia kwa waathiriwa

Afariki baada ya kubugia pombe ya asali

adminleo