Afariki baada ya kubugia pombe ya asali

Na PETER MBURU

MWANAMUME kutoka kijiji cha Ntoombo, eneo la Tigania Magharibi katika Kaunti ya Meru alifariki Jumapili, huku wenzake watano wakilazwa hospitalini baada ya kunywa pombe ya kutengenezewa nyumbani kwa asali.

Wanne kati ya watano hao ambao walikuwa wamelazwa katika hospitali ya kaunti ndogo ya Miathene waliruhusiwa kwenda nyumbani, lakini mwanamke ambaye hali yake haikuwa shwari bado anaendelea kupokea matibabu.

Msaidizi wa chifu eneo la Ntoombo Joseph Mutiga alisema kuwa mkazi alitengeneza pombe hiyo ya asali kisha akaitia ‘yisti’ kabla ya kuwakaribisha majirani kusherehekea.

Aliyekufa alifahamika kuwa Kunyanga M’Limung’I, chifu huyo akisema “Nashuku yisti ndiyo ilisababisha matatizo hayo.”

Kulingana na wakazi, punde tu baada ya kunywa, sita hao walianza kutapika na hali ilipozidi unga ndipo wakakimbizwa hospitalini kwa matibabu.

“Mgema alitia yisti katika pombe hiyo na huenda hilo ndilo lilisababisha kutapika huko na kuendesha,” akasema Bw Daniel Gitonga, jirani.

Wakazi walilalamika kuhusu ongezeko la unywaji wa pombe haramu katika eneo hilo, wakilaumu wasimamizi wa serikali kwa kuzembea kazini.

Wengi wa wakazi walikuwa wamelewa saa za asubuhi, ishara ya jinsi pombe haramu zimezidi eneo hilo.

Habari zinazohusiana na hii