• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Utata kuhusu mpango wa kulazimisha kaunti kununua vifaa vya matibabu

Utata kuhusu mpango wa kulazimisha kaunti kununua vifaa vya matibabu

Na PETER MBURU

MPANGO tata wa Serikali Kuu kukata serikali za kaunti mabilioni ya pesa kwa lazima ili kufadhili ununuzi wa vifaa vya afya unaonekana kuibua migawanyiko katika Bunge la Seneti.

Baada ya magavana kulalamika kuwa walishurutishwa kutia sahihi kandarasi za kusambaziwa vifaa hivyo ambavyo vingi havitumiki, Seneti kupitia Kamati yake ya Afya ilianzisha uchunguzi kuhusu jinsi mpango huo ulifanywa na matokeo yake.

Hata hivyo, wiki chache tu baada ya uchunguzi huo kuanzishwa, madai yaliibuka jana kuwa kuna mpango wa kuundwa kwa kamati ya muda kuchunguza jinsi serikali ilifanya mpango huo, jambo ambalo wanachama wa Kamati ya Afya hawakulifurahia.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, seneta wa Trans Nzoia Michael Mbito Jumanne aliongoza wanachama wake kupinga mpango wa kuundwa kwa kamati ya muda kuchunguza kuhusu mpango huo, akisema kamati yake haijashindwa na kazi.

Bw Mbito alisema tayari kamati yake inaendeleza uchunguzi huo, na kuwa imezuru katika baadhi ya kaunti, kuhoji magavana na kujionea vifaa vinavyorejelewa.

“Tayari tumeanza kuzuru katika kaunti, tumewahoji baadhi ya magavana, wagonjwa na washikadau wengine na kuzuru katika vituo vya afya kujionea vifaa husika. Tunapanga kukutana na maafisa katika wizara ya afya aidha kuwahoji kuhusiana na mpango huo,” akasema seneta Mbito.

Seneta huyo pamoja na wanachama wa kamati yake walisisitiza kuwa walikuwa wakipinga kutwaliwa kwa jukumu la uchunguzi huo mikono yao, wakiongeza kuwa hata endapo bunge lingeamua kufanya hivyo, wangeeleza pingamizi zao wazi.

“Hii kamati inashughulikia suala hili na itaendelea kulishughulikia kwani ni jukumu lake. Kuna baadhi ya maseneta ambao wanataka kuundwe kamati ya muda kulishughulikia kwa sababu zao wenyewe lakini hatutakubali, tunapinga hatua ya aina hiyo,” akasema.

Mjadala huu uliibuka baada ya kikao ambacho kamati hiyo iliandaa na maafisa kutoka Shirika la Kutathmini Masuala ya Kiuchumi (IEA) kuhusu suala la mpango wa vifaa hivyo vya afya, maseneta wakidai kuna mpango wa kuyeyusha mambo kazi ambayo wamefanya.

“Kuna maswali mengi muhimu ambayo sharti yaulizwe katika mradi huu kwani usiporekebishwa unaweza kuwa mmoja kati ya sakata ambazo zimeshuhudiwa. Ni jukumu la serikali kuu kutoa huduma za afya katika kaunti?” akauliza seneta wa Kisumu Fred Outa.

Lakini wakati wa kikao cha bunge Jumanne alasiri, baadhi ya maseneta walieleza kuwa kamati hiyo imeshindwa kufanya kazi yake, wakilitaka Bunge la Seneti kuingilia kati kutatua hali.

“Ni dhahiri kuwa kamati haijafanya kazi yake ipasavyo, itabidi Seneti kuingilia kati katika suala hili,” akasema seneta wa Makueni Mutula Kilonzo Jnr.

Kamati hiyo ilisema inatarajia kuwasilisha ripoti kuhusu uchunguzi huo ndani ya siku 60.

You can share this post!

Osotsi atimuliwa ANC

Tulizika vidoli kuwazima waliotaka kunyakua ardhi yetu,...

adminleo