Habari Mseto

Baadhi ya wadau vita dhidi ya dawa za kulevya walaumu mahakama

May 15th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MWANGI MUIRURI

WADAU katika vitengo vya kiusalama Mlima Kenya wameteta kuwa baadhi ya mahakama za eneo hilo zinahujumu vita dhidi ya mihadarati.

Haya yalijiri Jumanne katika kikao spesheli kilichoandaliwa na mshirikishi wa usalama eneo la Kati, Wilfred Nyagwanga katika Mkahawa mmoja Mjini Nyeri na ambapo changamoto za kupambana na kero hiyo ya mihadarati ziliwekwa wazi kujadiliwa.

Vitengo kadha vya kiusalama kutokana na hali hiyo vimewataka Jaji Mkuu David Maraga na mkurugenzi wa mashtaka ya umma (DPP) Noordin Haji sawia na Rais Uhuru Kenyatta waagize maafisa wa mahakama katika eneo hilo watilie mkazo kero kuu ya mihadarati katika jamii.

Mwenyekiti wa mpango wa usalama wa Nyumba 10 Bw Joseph Kaguthi alisema amepokea malalamishi kutoka kwa wenyeji kuwa baadhi ya maafisa wa mahakama hiyo huwa na uhusiano wenye shaka na walanguzi wa dawa za kulevya.

“Kisa cha hivi karibuni ambacho kimezidisha shaka zetu ni cha mshukiwa mmoja kutoka Mji wa Maragua ambaye kwa miaka miwili sasa ako na kesi 21 za ulanguzi wa mihadarati katika mahakama hiyo,” akasema.

Huku maafisa katika afisi ya msajili wa mahakama hizo wakisemwa kutotilia maanani tetesi za maafisa wa kiusalama kuhusu kuachiliwa kwa bodi kwa mshukiwa huyo katika kesi hizo zote, Kaguthi alisema kuwa hali kama hiyo haionyeshi idara ya mahakama ambayo iko tayari kuwajibikia jamii katika kupambana na athari za wafanyabiashara wa bidhaa za ‘mauti’.

“Hebu tutumie umakinifu wa mawazo hapa: Mshukiwa wa mihadarati anawasilishwa mahakamani mara 21 na katika harakati hizo zote, mahakama hiyo haitambui hatari iliyoko katika jamii kwa kuwa amedhihirisha hawezi kukoma kuiuza na huwa inamwachilia tu. Si basi tunaweza sema mahakama hiyo ni mshirika wa mihadarati?” akasema.

Kwa upande wake, aliyekuwa Mwenyekiti wa mamlaka ya kupambana na mihadarati (Nacada) Bw John Mututho alisema amepata malalamishi kuhusu mahakama, akisema kuwa ni suala la kuvaliwa njuga kati ya vitengo vya kiutawala, mahakama ikiwa moja yavyo.

“Rais Kenyatta ameagiza Nacada ifanye bidii kumaliza utumizi wa mihadarati hapa nchini. Lakini ni aibu kuwa licha ya kuwasukuma maafisa wa polisi kukabiliana na walanguzi, mahakama zetu zimekuwa ngome za kuwapa hifadhi washukiwa,” akasema Nyagwanga.

Bw Kaguthi alisema kuwa atamwandikia barua ya malalamishi Rais Kenyatta na kisha ainakili kwa afisi ya DPP pamoja na ile ya Jaji Mkuu akitaka kuelezewa kuhusu hitilafu hiyo.

Kamanda wa polisi wa Kaunti ya Murang’a Bw Joseh Kinyua alisema kuwa washukiwa wengi hawaadhibiki kutokana na maamuzi ya baadhi ya mahakama za eneo hilo.

“Tumejaribu hata kuwasilisha rekodi za bodi zote ambazo zimekabidhiwa baadhi ya washukiwa ambao wako nje na bodi za mahakama tukilenga kushawishi mahakama hizo zitambue kuwa washukiwa hao ni watu ambao  hawawezi kubadili mienendo yao lakini sisi hushtukia wako nje tena,”  akasema.