• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 6:50 PM
Unyakuzi wa ardhi watishia kuangamiza makavazi na turathi

Unyakuzi wa ardhi watishia kuangamiza makavazi na turathi

NA KALUME KAZUNGU
 
MAKAVAZI na turathi nyingi za kitaifa ambazo ni vivutio vikuu vya watalii kaunti ya Lamu ziko kwenye hatari ya kuangamia kufuatia ongezeko la maskwota na wanyakuzi wanaovamia ardhi zilizotengewa makavazi hayo.
 
Naibu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Usimamizi wa Turathi na Makavazi nchini (NMK) Ukanda wa Pwani, Bw Athman Huseein, alisema Lamu imeshuhudia ongezeko la sehemu za makavazi kuvamiwa na maskwota na wanyakuzi, hatua ambayo aliitaja kuchangiwa na kuwepo kwa Mradi wa Bandari Mpya ya Lamu (LAPSSET) eneo hilo.
 
Anasema LAPSSET imepelekea watu wengi kutoka mbali na karibu kutafuta makazi Lamu, hivyo kupelekea ongezeko la uvamizi na unyakuzi wa ardhi, ikiwemo zile za makavazi.
 
Bw Hussein alitaja makavazi kama vile Pate kuwa miongoni mwa sehemu ambazo tayari zinaendelea kunyakuliwa.
 
Sehemu nyingine za makavazi ni Takwa, Manda, Shanga na Siyu.
 
Alisema NMK tayari imefanya juu chini na kupata mgao wa fedha utakaosaidia kutunza makavazi na turathi za Lamu zisiingiliwe na wanyakuzi.
 
Bw Hussien aidha aliitaka serikali kuteka fedha zaidi zitakazotumika kuweka seng’eng’e kuzingira ardhi za makavazi.
 
Alitaja Lamu kuwa kaunti yenye utajiri mwingi zaidi wa makavazi na turathi ikilinganishwa na kaunti zote 47 za hapa nchini.
 
“Ujio wa LAPSSET umezidisha wingi wa watu wanaotafuta makao Lamu. Hii imepelekea donda sugu la uskwota kuongezeka. Wanyakuzi wa ardhi nao wanazidi kuendeleza maovu yao.
“Inasikitisha kwamba maeneo ya makavazi na turathi pia yameanza kulengwa na kunyakuliwa. Tuko mbioni kulinda makavazi na turathi hizo lakioni cha msingi ni serikali kupiti tume ya ardhi (NLC) kutoa hatimiliki za ardhi kwa maeneo yote ya makavazi na turathi Lamu,” akasema Bw Athman.
 
Kauli yake iliungwa mkono na Afisa Msimamizi wa Makavazi na Turathi za Lamu, Bw Mohamed Mwenje, aliyesema baadhi ya wanaoendeleza juhudi za kutunza makavazi na turathi wamekuwa wakilengwa na kukabilkiwa na jamii zinazodai sehemu za makavazi ndio makao ya wazee wao wa tangu jadi na kwamba wako na haki ya kuishi kwenye sehemu hizo.
 
“Mahali kama vile Pate imekuwa tatizo sisi kufanikisha juhudi za kutunza turathi. Jamii imekuwa ikipinga kabisa juhudi zetu za kutunza ardhi za makavazi. Hii ndiyo sababu wakazi wametwaa sehemu kubwa ya ardhi na kuikalia,” akasema Bw Mwenje.

You can share this post!

Ongwae akaidi CoG na kuhudhuria kikao bungeni

Ashangaza kujiua baada ya kunyimwa chakula na mke

adminleo