• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
SRC yataka wabunge warejeshe marupurupu

SRC yataka wabunge warejeshe marupurupu

Na DAVID MWERE
TUME ya Kusimamia Mishahara ya Watumishi wa Umma (SRC), imetishia kushtaki wabunge ili korti iwashinikize kurejesha fedha walizojiongezea za marupurupu ya kodi ya nyumba.
Mwenyekiti wa SRC, Lyn Mengich Jumatano alisema wabunge walijiongezea marupurupu hayo bila kushauriana na tume yake.
Alisema tume ya SRC ndiyo imepewa mamlaka ya kutathmini nyongeza ya mishahara na marupurupu ya watumishi wote wa umma.
SRC imetangaza hatua hiyo baada ya wabunge na maseneta kujiongezea marupurupu ya Sh250,000 kila mwezi kwa ajili ya kodi ya nyumba.
Kila mbunge alipokea zaidi ya Sh1.2 milioni juu ya mshahara wa Aprili kwani walilipwa malimbikizi ya marupurupu ya nyumba ya kuanzia Oktoba, mwaka jana.
Kulingana na SRC, nyongeza hiyo ya marupurupu ni haramu na wabunge wanafaa kurejesha fedha hizo.
“Tumechukua hatua hiyo ili kuhakikisha kwamba mishahara yote inayolipwa bila idhini ya SRC inakomeshwa. SRC itaenda mahakamani ili wabunge walazimishwe kurejesha hela hizo walizopokea kiharamu,” akasema Mengich.
Spika wa Bunge la Kitaifa, Justin Muturi ambaye ni mwenyekiti wa Tume ya Huduma za Bunge (PSC), ambayo hushughulikia masilahi ya wabunge, alilitea nyongeza hiyo akisema kuwa wabunge wanastahili kulipwa marupurupu hayo.
“Tume ya PSC iliamua kuwapa wabunge marupurupu ya nyumba kwa mujibu wa uamuzi wa mahakama uliotolewa na Jaji Chacha Mwita mnamo Oktoba 5, 2018, ambaye alisema kuwa watumishi wote wa umma wanastahili kupewa marupurupu hayo,” akasema Bw Muturi.

You can share this post!

HUDUMA NAMBA: Vijana Baringo wataka walipwe kabla ya...

Maraga asikitika mahakama nchini zinatumiwa kama tambara...

adminleo