Teknolojia pekee ndiyo itaokoa bara la Afrika – Rais
CHARLES WASONGA na PSCU
RAIS Uhuru Kenyatta Jumatano alitoa wito kwa nchi za Afrika kuupa kipaumbele ushirikishi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT) katika mipango yao ya maendeleo kwani fani hiyo ina uwezo mkubwa wa kuimarisha uchumi wa mataifa hayo.
Rais alisema haya alipozindua mpango wa taifa la Kenya wa kustawisha uchumi kwa kutumia mfumo wa dijitali kwa wawekezaji na viongozi wa mataifa wanaohudhuria mkutano wa mwaka huu wa kuchochea mageuzi barani Afrika, uliofanyika jijini Kigali, Rwanda. Mpango huo unatambulika kimombo kama; “Smart Africa Initiative”
Viongozi wa mataifa waliohudhuria uzinduzi huo ni mwenyeji; Rais Paul Kagame na Rais wa Mali, Boubakar Keita. Rais huyo wa Rwanda ndiye mwenyekiti sasa wa mpango huo unaolenga kubuni soko moja la kidijitali katika bara hilo kufanikisha biashara na uwekezaji.
Mkakati wa kidijitali wa taifa la Kenya chini ya mada, “Kuthibiti Uwezo wa Mabadiliko nchini Kenya” ulizinduliwa mbele ya zaidi ya wajumbe 4,000 miongoni mwao maafisa wa serikali, watunga sera na maongozi, wabunifu na wawekezaji katika nyanja ya tekniolojia ambao wanakutana kujadili jinsi raslimali za ICT zinazvyoweza kutumika kuimarisha uchumi wa mataifa ya Afrika.
Kupitia mkakati huo, serikali inakusudia kuimarisha mchango teknolojia ya habari na mawasiliano kwa uchumi kupitia matumizi ya teknolojia katika utaratibu wa kibiashara.
Kama bingwa wa matumizi ya mitambo ya kidijitali katika bara Afrika, Rais Kenyatta aliuambia mkutano huo kwamba Kenya imewekeza sana katika mfumo wa kidijitali na inashirikiana na mashirka mengine kuhakikisha mfumo huo umesambazwa kote kwa njia ya uadilifu.
“Maono yetu ni kwamba katika miaka mitano ijayo, kila sehemu ya nchi itakuwa imepata mfumo wa kidijitali na hivyo kuwaruhusu raia kushiriki na kufaidi kwayo,” akasema Rais Kenyatta.
Rais pia alizungumzia kuhusu umuhimu wa vijana katika uchumi wa kidijitali barani Afrika akisema Kenya imeratibu mpango maalumu unaokusudiwa kuwapa vijana shime kwa kuwapa ujuzi katika nyanja za ICT.
“Tunawahimiza vijana kuwa msitari wa mbele na kujitosa katika soko la biashara ya kidijitali kupitia mpango wa ajira ambao umewasaidia wengi kupata kazi za mtandao,” Rais Kenya akaeleza.
Mapema kabla ya kongamano hilo, Rais Kenyatta alitembelea vibanda mbali mbali vilivyowasilisha bidhaa zao mbali mbali ikiwemo kibanda cha Kenya. Bidhaa hizo zinatumika kuimarisha na kutumia kwa njia bora teknolojia hiyo katika sekta mbali mbali za kiuchumi ikiwemo katika sekta ya kilimo.
Rais Kenyatta pia alisema kuwa Kenya iko mstari wa mbele katika kuendeleza matumizi ya teknolojia katika uimarishaji uchumi wa Afrika akitoa mfano wa uvumbuzi wa njia ya kutuma na kupokea pesa kwa simu ya mkono, maarufu kama MPESA. Alisema uvumbuzi huu ni ni dhihirisho la nafasi chungu nzima zilizoko katika bara hili za kutumia ICT kufanisha shughuli za kuichumi.