• Nairobi
  • Last Updated March 19th, 2024 1:13 PM
UFUGAJI: Masuala muhimu kuzingatia kabla kuanza kufuga kuku

UFUGAJI: Masuala muhimu kuzingatia kabla kuanza kufuga kuku

Na SAMMY WAWERU

UFUGAJI wa kuku ni miongoni mwa sekta ambapo wengi wameingilia ili kujiinua kimapato.

Wanafugwa kwa ajili ya nyama na mayai, mazao muhimu yaliyosheheni Protini.

Pia, kuna wanaofuga kuku kwa minajili ya kuchangamsha maskani yao.

Kinyesi cha ndege hawa wa nyumbani ni mbolea inayoorodheshwa kuwa miongoni mwa hai na hutumika katika kilimo.

Hivyo basi, wanaofuga na pia kufanya kilimo huitumia kukuza mimea.

Ili kufanikisha ufugaji wa kuku, mkulima anapaswa kuzingatia masuala kadha wa kadha.

Bw Okuta Ngura, ambaye ni mtaalamu wa masuala ya ndege hasa wa nyumbani, anasema lishe, vifaa vya kula, na makazi ndivyo vigezo muhimu kutilia maanani kabla ya kuanza kufuga kuku.

Gharama ya kuendesha biashara hapa nchini inaendelea kukwea mlima, na hii imeathiri sekta nyingi, kilimo na ufugaji ikiwemo.

Bi Margaret Maina, mfugaji wa kuku wa kienyeji wa kisasa Kaunti ya Kiambu. Picha/ Sammy Waweru

“Hushauri wakulima kutumia baketi mahala pa vifaa vya kuwatilia chakula na maji, ili kupunguza gharama ya kununua vile maalumu,” asema Ngura.

Kulingana na mtaalamu huyu ni kwamba haja ipo mfugaji kujua atakaponunua chakula chenye madini kamilifu, na kwa bei nafuu. “Ni masuala wewe kama mfugaji unapaswa kufanya utafiti kabla kuanza,” asisitiza.

Utafiti unaweza ukafanywa kwa kuzuru waliofanikisha ufugaji wa kuku, mitandao ambapo ina habari za wachangiaji waliofanikiwa na hata wataalamu.

Maonyesho ya kilimo na ufugaji, kuhudhuria semina au warsha zilizoandaliwa na wadau husika, pia ni baadhi ya njia zinazonoa mfugaji chupikizi.

Ni kupitia hafla za aina hiyo mfugaji atapata fursa ya kutangamana na wataalamu.

“Teknolojia hukua kila uchao na kutoa mwelekeo mpya wa kuimarisha ufugaji. Hafla hizo hunoa wakulima na wafugaji,” ashauri Bw Ngura.

Hata hivyo, anaonya mfugaji awe makini kwa mafunzo anayopata kutoka kwa wakulima na mitandao.

“Ni muhimu kuthibitisha maelezo unayopata kwa wataalamu,” ashauri.

Margaret Maina, mfugaji wa kuku wa kienyeji wa kisasa Kiambu, anasema kabla ya kuvalia njuga ufugaji wa kuku alifanya utafiti wa kutosha.

“Nilianza kufuga kuku 2016, na nilitangulia kufanya utafiti. Ingawa nimepitia changamoto mbalimbali, fahari ninayojionea ni kwamba nimepiga hatua katika azma yangu,” asema Bi Maina.

Mfugaji huyu ana zaidi ya kuku 200 wa mayai na nyama, almaarufu ‘kuroilers’. Mbali na chakula maalum cha kuku, pia huwapa mahindi na masalia ya chakula cha binadamu.

Bi Maina anaendelea kueleza kwamba utafiti wake pia ulijumuisha soko atakalopeleka mazao.

Katika siku za hivi karibuni wafugaji wa kuku Kenya wamekuwa wakilalamikia kuwepo kwa mayai na kuku wa nyama kutoka nje, suala ambalo limetishia soko la mazao ya humu nchini.

Bi Margaret Maina, mfugaji wa kuku wa kienyeji wa kisasa Kaunti ya Kiambu. Picha/ Sammy Waweru

Changamoto hii imetokana na hatua ya serikali kufungua mipaka ya mataifa ya Afrika Mashariki, na kuruhusu nchi wanachama kuendesha biashara huru.

“Unapoanza kufuga kuku unapaswa kujua soko unalolenga na ni kina nani kwa mujibu wa mazao kama vile; mayai, vifaranga, nyama au kuku waliokomaa,” aelezea Bi Maina, kauli inayotiliwa mkazo na Bw Okuta Ngura, mtaalamu.

“Mawakala wamekuwa kero kuu kwa wakulima na wafugaji, utafiti wa soko utakuwezesha kujua utakapouza mazao. Ni mawakala wachache mno wasiopunja,” anasema mdau huyu.

Mtaalamu huyu wa kuku anahimiza haja ya kujua magonjwa na vimelea vinanvyoathiri kuku.

Vifaranga wanapaswa kuchanjwa kwa mujibu wa maelekezo ya daktari wa mifugo au mtaalamu.

Unapoona kuku wana udhaifu, usisite kuhusisha mtaalamu wa mifugo ili kutambua ndwele wanayougua kwa ajili ya matibabu.

Usafi katika vizimba, vifaa vya kuwaitilia chakula na maji, pamoja na mazingira yao, unafaa kuwa wa hadhi ya juu ili kudhibiti maambukizi ya magonjwa na vimelea kama viroboto.

Yote tisa, ya kumi unahimizwa kufuga kuku walioidhinishwa na tasisi ya kitaifa ya utafiti wa kilimo na ufugaji nchini (Karlo) . Bw Ngura anatahadharisha wafugaji kwamba kuna kuku ambao hawajaafikia vigezo vinavyohitajika.

Hilo hasa hutokana na kujamiisha kuku ambao mayai yake yametagwa, kutotolewa au kuanguliwa na koo mmoja. Unashauriwa kutafuta mayai au kuku kutoka kwa wafugaji tofauti ili kuepuka kuwazalisha kutoka kwa ‘familia’ moja (inbreeding), suala linalofanya ndege kuwa dhaifu.

You can share this post!

Kenya tayari kutetea ubingwa wa voliboli ya wanawake Afrika

MAPISHI: Keki ya karoti

adminleo