• Nairobi
  • Last Updated March 19th, 2024 6:55 AM
Mshukiwa mkuu wa mauaji ya Matungu anyakwa

Mshukiwa mkuu wa mauaji ya Matungu anyakwa

Na WAANDISHI WETU

WAPELELEZI wamemkamata mshukiwa sugu ambaye ni mmoja wa washukiwa wakuu wanaohusishwa na mauaji katika Kaunti Ndogo ya Matungu na eneo la Kilingili, Magharibi ya Kenya.

Boniface Gubimiru almaarufu Guga mwenye umri wa miaka 24, alikamatwa na maafisa wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) Ijumaa usiku na kuzuiliwa katika kituo cha polisi cha Mbale, kwa mujibu wa maafisa.

Operesheni ya kusaka wahalifu wa magenge hayo yanayohangaisha raia inasimamiwa moja kwa moja kutoka makao makuu ya DCI jijini Nairobi.

Mshukiwa mwingine, Kelson Lienga almaarufu Kevin Lienga alikamatwa Jumatano, Mei 15 na kupelekwa katika kituo cha polisi cha Mbale ambako anaendelea kuhojiwa.

DCI wanaamini wawili hawa ndio viongozi wa magenge ya wahalifu wanaosababisha mauaji na majeraha kwa wakazi wa maeneo ya Magharibi.

Wakati huo huo, polisi walifichua kuwa wanapanga kuwafungulia mashtaka ya uchochezi wanasiasa wanne wanaohojiwa kuhusiana na visa vya mauaji ya wanakijiji na wahalifu katika eneobunge la Matungu, Kaunti ya Kakamega.

Kaimu Mkuu wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (CID) Shem Nyamboki jana alisema wanasiasa hao; Seneta wa Kakamega Cleophas Malala, aliyekuwa Waziri wa Michezo Rashid Echesa, Mbunge wa Matungu Justus Murunga na Diwani wa wadi ya Mayoni Libinus Oduori pia watashtakiwa na makosa yanayohusiana na ufadhili wa magenge wa wahalifu.

Ukusanyaji habari

Bw Nyamboko alisema wapelelezi wanakusanya habari zaidi kuhusu shughuli za magenge hayo ambapo kufikia sasa yametekeleza mauaji ya kinyama ya zaidi ya watu 10 katika eneo hilo.

Mbw Malala, Echesa na Oduori walikamatwa Ijumaa jioni na wakazuiliwa katika seli za vituo mbalimbali vya polisi. Bw Murunga alikamtwa jana asubuhi baada ya kujiwasilisha katika kituo cha polisi kilichoko karibu.

Hata hivyo, wakili wa Bw Malala amelalamika kwamba mteja wake amenyimwa haki ya kutembelewa na watu wa familia yake na kupata huduma za afya “kwani anaugua kisukari na shinikizo la damu”.

Licha ya kuwa katika kambi ya makao makuu ya polisi ukanda wa Nyanza mjini Kisumu, wakili wake Charles Malala alisema kuwa hawakuruhusiwa kumwona mwanasiasa huyo.

You can share this post!

Matiang’i aongoza sherehe ya kumuaga Boinnet

ODM yamtetea Raila kuhusu sakata ya dhahabu

adminleo