Habari Mseto

Kaunti kutwaa usimamizi wa kiwanda cha Mumias Sugar

May 19th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na SHABAN MAKOKHA

HALI ya matumaini imerejea miongoni mwa wakulima wa miwa katika eneo la Mumias, Kaunti ya Kakamega, baada ya serikali ya kaunti hiyo kutangaza kuwa itachukua usimamizi wa shughuli za kiwanda cha Mumias Sugar.

Gavana Wycliffe Oparanya alisema kuwa serikali yake itachukua usimamizi huo kutoka kwa bodi ya sasa ya wakurugenzi.

Bw Oparanya alisema kuwa alifanya uamuzi huo baada ya bodi hiyo kutoa pendekezo la kukodishwa kwa baadhi ya mali ya kiwanda hicho kama maeneo ya kuzalishia maji na umeme, uwanja wa mchezo wa gofu, shule, nyumba zaidi ya 2,500 na chumba cha kuwapokea wageni.

Akizungumza katika kikao maalum cha wadau katika mkahawa mmoja mnamo Ijumaa, Bw Oparanya alisema kuwa matumaini yake ni kuona kiwanda hicho kikirejelea shughuli zake kabla ya kumalizika kipindi chake kama gavana.

“Nilipokea malalamishi kutoka kwa wakulima wa miwa, wakinitaka kuingilia kati ili kusimamisha mpango wa kuuza baadhi ya mali yake. Niliwahakikishia kuwa hakuna chochote kitakachouzwa bila idhini yangu,” akasema.

Akaongeza: “Hatutawaruhusu wakurugenzi kuuza mali ya kampuni kisiri bila kuiarifu serikali ya kaunti ama wakulima. Tuko tayari hata kwenda mahakamani, kukiwa na haja.”

Kampuni hiyo ilikuwa imeweka tangazo la kukodisha baadhi ya mali ya kampuni hiyo, lakini ikasitisha mpango huo baada ya usimamizi wake kukutana na Bw Oparanya jijini Nairobi mnamo Mei 7. Wakulima wengi na serikali ya kaunti walieleza kutoridhishwa na mpango huo, huku wakiionya bodi dhidi ya kuingilia mali yake.

Mkutano huo ulihudhuriwa na watu 21, wakiwemo wale iliyo na madeni nao.

Baadhi ya masuala yaliyopitishwa ni kuwa serikali ya kaunti inapaswa kubuni kundi maalum kusimamia shughuli za kiwanda hicho na hakuna jambo au uuzaji wowote wa mali utakaofanywa bila kumhusisha gavana na serikali yake. Mkutano huo pia ulipitisha kuwa kiwanda hicho kinapaswa kushirikiana na serikali kwa ustawishaji wa miwa.

Bw Oparanya alitangaza kuwa maafisa maalum wa kaunti watatumwa kuhakikisha kuwa hakuna mali yake yoyote itauzwa.

“Nitafanya kikao maalum na Rais Uhuru Kenyatta na Waziri wa Kilimo ili kuhamisha asilimia 20 ya hisa zinazomilikiwa na serikali ya kitaifa kwa serikali ya kaunti,” akasema.