JAMVI: Sababu kuu za Ruto kuhepwa na wandani
Na CHARLES WASONGA
JAPO Naibu Rais William amekuwa mbioni akijaribu kujiimarisha kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa 2022, baadhi ya wafuasi wake wameanza kumtoroka huku wengine wakiingiwa na baridi hali ambayo imeleta wasiwasi katika kambi yake maarufu kama “Team Tanga Tanga.”
Kinaya ni kwamba ni katika ngome yake ya Rift Valley ambapo baadhi ya wanasiasa wengi wameamua kujitenga na kampeni za kumpigia debe na kuhamia vyama vingine au huku wengine wakiamua kuzipa kisogo kampeni hizo.
Katika kaunti yake ya Uasin Gishu ni Mbunge wa Kapseret Oscar Sudi na mwenzake wa Soy Caleb Kositany ambao bado wanaendeleza kampeni hizo. Lakini viongozi wengine wakiongozwa na Gavana Jackson Mandago na Seneta Margaret Kamar katika siku za hivi karibuni hawaonekani wakiandama na Dkt Ruto katika ziara zake sehemu mbalimbali nchini.
Viongozi wengine kutoka kaunti hiyo ambao wamejitenga na kampeni za Dkt Ruto ni wabunge, Glady Shollei (Mbunge Mwakilishi wa wanawake), William Chepkut (Ainabkoi), Silas Tiren (Moiben), Swarup Mishra (Kesses) na Janet Sitienei anayewakilisha eneobunge la Turbo anakotoka Dkt Ruto.
Wanasiasa wengine ambao wamemtoroka Naibu Rais ni mfanyabiashara mashuhuri kaunti ya Uasin Gishu Hezekiel Kiprop Bundotich, maarufu kama Buzeki na Gavana wa Elgeyo Marakwet Alex Tolgos, wakilalamikia kile walichotaja kama kudhalilishwa na wanasiasa wanaomzingira Dkt Ruto.
Buzeki ametangaza kujiunga na Chama cha Mashinani (CCM) chake aliyekuwa Gavana wa Bomet Isaac Ruto huku Tolgos akionekana kujibanza kwa KANU inayoongozwa na Gideon Moi.
Katika eneo la Mlima Kenya kasi ya kampeni ya Ruto sasa zinaonekana kupungua huku wabunge Ndindi Nyoro (Kiharu) na Kimani Ichungwa (Kikuyu) wakionekana kama ambao ndio wamesalia shakiki katika jahazi la Team Tanga Tanga.
Wabunge kutoka eneo hilo tuliozungumza nao walifichua kwamba wameamua kupunguza kasi yao ya kumpigia debe Dkt Ruto kutokana “vitisho” kutoka maafisa fulani wa serikali.
“Tumeamua kutuliza baada ya watu wengine kuanza kueneza propaganda zenye nia mbaya. Watu hao sasa wanashirikiana na maafisa fulani wa serikali kuendesha siasa dhidi yetu,” akasema mmoja ambaye aliomba tulibane jina lake.
Mwezi uliopiga Mabw Nyoro, Ichung’wa, Kimani Ngunjiri (Bahati), Gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu na Seneta wa Nakuru Susan Kihika walipokonywa walinzi kwa muda katika kile kilichoonekana kama hatua ya kuwaadhibu kwa kuunga mkono ndoto ya Dkt Ruto ya kuingia Ikulu 2022.
Na hivi majuzi kumekuwa na mpango wa kuwaondoa wafuasi wa Team Tanga Tanga kutoka nyadhifa wanazoshilia katika kamati mbalimbali za bunge katika kile kinachoonekana kama hatua ya kuwaadhibu kwa kukaidi wito wa Rais Uhuru Kenyatta kwamba wakomeshe kampeni za mapema za urais.
Mbunge Mwakilishi wa Murang’a Sabina Chege alithibitisha kufahamu kuhusu mipango hiyo lakini akashikilia kuwa “hatutakubali kutishwa kwa sababu ya msimamo wetu”
“Kile ambacho kitaweza kunitia woga zaidi ni ikiwa wakazi wa Murang’a wataamua kunifuta kazi. Wajibu wa kuhutumu katika kamati za bunge huwa ni wa ziada tu, msukumo ukiwa ni moyo wa kujitolea” anasema mbunge huyo ambaye ni mwenyekiti wa Kamati ya Bunge la Kitaifa kuhusu Afya.
Na katika eneo la Pwani kati ya zaidi ya wabunge 10 ambao wamekuwa wakipiga magoma ya kumnadi Dkt Ruto kama anayefaa kumrithi Rais Kenyatta ni Mbunge wa Malindi Aisha Jumwa pekee anayeendeleza kampeni hizo kwa nguvu na bidii.
Wenzake kama vile Sharrif Alwy (Lamu), Michael Kingi (Magarini), Owen Baya (Kilifi North), Ali Mbogo (Kisauni), Badi Twalib (Jomvu), Benjamin Tayari (Kinango), Paul Katana (Kaloleni) na wengine wameonekana kujitenga na “Team Tanga Tanga”.
Sasa wanasiasa kutoka Rift Valley na wadadisi sasa wanadai kuwa hali hii ya wandani wa Dkt Ruto kuonekana kumtoroka pia inachangiwa na masaidizi wake, Farouk Kibet, wanaosema amekuwa akiwazuia viongozi kumfikia kwa urahisi.
Kwa zaidi ya miaka saba iliyopita Kibet amehudumu kama msaidizi wa Dkt Ruto na ndiye amekuwa akitoa kibali kwa wale wanaopania kumfikia kiongozi huyo afisini mwake jumba la Harambee House Annex, makazi yake rasmi Karen na maeneo mengine.
Kwa mfano, Buzeki, juzi alidai kuwa Bw Kibet amekuwa akiitisha hongo kutoka kwa watu wanaotaka kumwona Dkt Ruto.
Mwanasiasa huyo ambaye aliwania ugavana wa Uasin Gishu mnamo 2017 na kushindwa na Gavana wa sasa Jackson Mandago, alimshauri Naibu Rais kumfuka kazi Bw Kibet ikiwa anataka kushinda uchaguzi wa urais 2022.
“Farouk ni “mkusanyaji ushuru” ambaye amezoea kuitisha pesa kutoka wa watu wenye haja ya kumwona Dkt Ruto,” Bw Kibet alisikika akiwaambia wafuasi wake katika video iliyosambazwa katika mitandao ya kijamii Jumanne.
Zaidi ya watu 5,000 walifika nyumbani kwake, katika eneo la Ainabkoi, siku hiyo.
Ni wakati huo ambapo Bw Buzeki alitangaza kuwa amekihama rasmi chama cha Jubilee na kujiunga na chama cha CCM, akisema ndicho kinaweza kuendeleza masilahi ya jamii ya Wakenjin wala sio Jubilee.
Hata hivyo, Mbunge wa Soy Caleb Kositany amepuuzilia mbali madai ya mwanasiasa huyo akiyataja hayo madai kama yaliyokosa ukweli wowote.
“Naibu Rais Dkt William Ruto ni kiongozi wa kitaifa na hufikiwa na viongozi wote kwa urahisi, wa Jubilee pamoja na wale wa upinzani. Madai ya Buzeti hayana ukweli wowote kwani hakuna hata siku moja ambapo kiongozi yeyote amezuiwa kumwona,” akasema.
Mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Festus Biwott naye anasema Dkt Ruto anaachwa na wandani kutokana na hulka yake ya “kiburi na dharau kwa wanasiasa wenye misimamo tofauti”
Aidha, anasema kiongozi huyo alikosana na baadhi ya wabunge kutoka eneo lake la Rift Valley kutokana na siasa za zao la mahindi mwaka jana.
“Hatua ya kupuuzilia mbali watetezi wa wakulima na kupendekeza kuwa wakulima waingilie kilimo cha mazao mengine kama parachichi haikufaa ikizingatiwa kuwa mahindi ndicho kitega uchumi kikuu kwa wakazi wengine Rift Valley,” akasema.
Anamshauri Dkt Ruto kuelekeza juhudi zake za kuunganisha ngome yake kisiasa kwanza kabla ya kuendeleza kampeni za kusaka uungwaji mkono kutoka maeneo mengine kuelelekea uchaguzi mkuu wa 2022.