Wakazi wa Zimmerman waahidiwa hatimiliki
Na SAMMY WAWERU
SERIKALI ya Kaunti ya Nairobi inashirikiana na serikali kuu kuwapa wamiliki wa ploti za mradi wa Zimmerman Settlement Scheme hatimiliki za mashamba.
MCA wa Zimmerman, Pius Mwaura amesema mikakati ya kupata stakabadhi na vyeti hivyo muhimu imeanza.
Akihutubu katika mkutano na wamiliki wa ploti za mradi huo unaosemekana kuwa wa maskwota na ulioko pembezoni wa Thika Super Highway, Bw Mwaura aliwahimiza kushirikiana na ofisi ya mradi huo ili kufanikisha hitaji hilo la kisheria.
“Mipango ya kutafuta hatimiliki imeanza. Tumewasiliana na tume ya kitaifa ya mashamba (NLC) na Wizara ya Ardhi, ili kila mwenye shamba au ploti hapa apate cheti. Tunachoomba ni ushirikiano wenu wa karibu,” akasema diwani huyo.
Mwezi uliopita, Aprili 16, ubomozi wa majengo eneo hilo ulifanyika na kufikia sasa haijabainika aliyeagiza kuutekeleza. Ilidaiwa agizo lilitoka katika ‘afisi ya hadhi ya juu zaidi serikalini’.
Bw Francis Kirima, mwenyekiti wa mradi huo alisema Zimmerman Settlement Scheme ilikadiria hasara ya mali yenye thamani zaidi ya Sh1 bilioni.
Mapema mwezi huu, gavana wa Nairobi Mike Sonko aliingilia kati na kuamuru shughuli ya ubomozi ikomeshwe mara moja.
“Mlipoona gavana amewasili, alitoka Ikulu kuzungumza na Rais Uhuru Kenyatta ambaye aliamuru ubomozi usimamishwe mara moja na suluhu ipatikane,” MCA Mwaura aliambia wamiliki hao mnamo wikendi.
Mwenyekiti, Bw Francis Kirima alisisitiza kuwa Zimmerman Settlement Scheme imemiliki mashamba ya mradi huo kihalali.
Alieleza kushangazwa kwake na walioagiza ubomoaji kufanyika, wakati Rais Kenyatta anajikakamua kuafikia ujenzi wa makazi bora na ya bei nafuu, ambayo ni mojawapo ya ajenda zake kuu nne.
“Tunashirikiana kuona Rais amehitimisha ajenda ya ujenzi wa makazi bora na ya bei nafuu. Tulikadiria hasara kubwa kama wamiliki,” alisema. Ofisi ya mradi huo pia ni miongoni mwa majumba yaliyobomolewa.
Suala la iwapo waliopata hasara watafidiwa, lingali kitendawili ikisemekana walioagiza ubomoaji kufanywa hawajajitokeza.
Wengine waliozungumza katika mkutano huo ni katibu wa mradi huo, anayejulikana kama Bw Brian.
Alisema usalama umeimarishwa ipasavyo hivyo basi ujenzi wa majumba uendelee bila wasiwasi wowte. “Kizungumkuti tulichokuwa nacho kimeangaziwa, tunaomba watu waendelee kujenga nyumba zao,” alisema.
Mradi huo una shamba lenye ukubwa wa karibu ekari 250, na si mara ya kwanza ubomoaji kufanyika. Mgogoro kuhusu umiliki wa mashamba ya mradi huo umekuwepo tangu 2002.
Halmashauri ya kitaifa ya mazingira (Nema) na ya ujenzi (NCA), ndizo ziliidhinisha ujenzi wa nyumba katika shamba hilo linalositiri maelfu ya watu.
Aidha, pia hupokea huduma za stima na maji chini ya kampuni ya kusambaza nguvu za umeme nchini, KP na Nairobi Water & Sewerage Company.
Serikali ya kaunti ya Nairobi mwaka uliopita, 2018, ilifanya ubomoaji wa majengo haramu na yaliyodaiwa kuwa katika ardhi ya umma. Ilishirikiana na Nema na mamlaka ya ujenzi wa barabara mijini.