Joho asusia hafla muhimu nyumbani kwa Ruto

Na LEONARD ONYANGO

GAVANA wa Mombasa Hassan Joho Jumatatu alisusia hafla iliyofanyika nyumbani kwa Naibu wa Rais William Ruto mtaani Karen, Nairobi.

Hafla hiyo ya kutia saini mkataba wa miradi ya maji kati ya kaunti nne za ukanda wa Pwani na Benki ya Dunia ilihudhuriwa na magavana Granton Samboja (Taita Taveta), Salim Mvurya (Kwale) na Amason Kingi (Kilifi).

Gavana Kingi alimtetea Bw Joho akisema kuwa alikosa kufika katika hafla hiyo kwa sababu alikuwa akifanya maandalizi ya hafla ya iftar ya jana jioni.

“Gavana wa Mombasa alitamani kushuhudia hafla hii lakini amebanwa na shughuli kuhusu hafla atakayokuwa nayo leo (jana) jioni),” akasema Bw Kingi.

Gavana Joho na Dkt Ruto ni mahasimu wa kisiasa.

Kaunti nne za ukanda wa Pwani zimepata afueni baada ya kupokea kitita cha Sh10.7 bilioni kwa ajili ya miradi ya maji kutoka kwa Benki ya Dunia.

Kupitia ufadhili huo, Kaunti ya Mombasa itapokea Sh3 bilioni, Kilifi Sh2.7 bilioni, Kwale sh2.5 bilioni, Taita Taveta Sh2.5 bilioni.

Kulingana na waziri wa Maji Simon Chelugui, sehemu ya fedha hizo itatumiwa kutoa mafunzo kwa kampuni za kusambaza maji katika kaunti hizo ili kuboresha huduma.

Bw Chelugui alisema kaunti nyingine zinazotarajiwa kunufaika na ufadhili huo wa miradi wa maji ni Wajir na Garissa.

“Benki ya Dunia imetenga kitita cha Sh30 bilioni kufadhili miradi ya maji safi na salama pamoja na usafi wa mazingira katika kaunti sita,” akasema waziri wa Maji.

“Serikali ya Kitaifa na Benki ya Dunia watasaidia serikali za kaunti kutekeleza miradi hiyo. Hata hivyo, nazisihi serikali za kaunti kuongeza hela za kufadhili miradi ya maji na usafi wa mazingira kuhakikisha kuwa kila Mkenya anapata maji safi na salama kufikia 2030,” akasema Bw Chelugui.

Wakizungumza baada ya hafla ya kutia saini mkataba wa maelewano kati ya kaunti hizo na Benki ya Dunia iliyofanyika nyumbani kwa Naibu wa Rais William Ruto mtaani Karen, Nairobi, magavana Granton Samboja (Taita Taveta), Salim Mvurya (Kwale) na Amason Kingi (Kilifi waliahidi kutumia fedha hizo kwa uadilifu.

“Tutahakikisha kwamba fedha hizo zinatumiwa katika miradi iliyopangiwa na hakuna hela zitakazofujwa,” akasema Gavana Samboja.

Alisema kampuni za kusambaza maji zitatwikwa jukumu la kuboresha miundomsingi ya kusambaza maji chini ya ufadhili huo.

Gavana Kingi alisema mradi huo utawezesha serikali ya Kaunti ya Kilifi kuafikia mpango wake wa kusambaza maji katika kila kijiji ili kuwaondolewa wakazi usumbufu wa kutembea umbali mrefu kusaka bidhaa hiyo.

“Ufadhili huo umetokea katika wakati ambapo tulikuwa tunaahitaji zaidi fedha za kufadhili miradi ya maji. Tutahakikisha kuwa hakuna fedha zinapotea wakati wa utekelezaji wa miradi hiyo,” akasema Gavana Kingi.

Naye Mvurya alisema mafanikio ya miradi hiyo itasababisha Benki ya Dunia kuwa na imani nao kaunti hizo hivyo kufadhili miradi zaidi.

Dkt Ruto alisema serikali za kaunti zimeachiwa jukumu la kutambua miradi ya maji itakayonufaika na ufadhili huo.

“Hatutaki watu kusema kwamba Benki ya Dunia au Serikali ya Kitaifa ndio walitambua miradi ya maji. Jukumu hilo limeachiwa serikali za kaunti,” akasema Naibu wa Rais.

Takwimu za Wizara ya Maji zinaonyesha kuwa ni asilimia 60 pekee ya maeneo nchini Kenya yana maji ya kutosha.

Wizara inalenga kuhakikisha kuwa asilimia 80 ya maeneo ya Kenya yanakuwa na maji safi na salama kufikia 2022 na asilimia 100 kufikia 2030.