• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Wakazi wa Gatundu Kaskazini wahimizwa wahame kutoka eneo la mradi wa maji wa Kariminu

Wakazi wa Gatundu Kaskazini wahimizwa wahame kutoka eneo la mradi wa maji wa Kariminu

Na LAWRENCE ONGARO

FAMILIA kadhaa za eneo la Gatundu Kusini zinaitaka serikali kuzifidia fedha baada ya kuhamishwa kutoka eneo la Kariminu.

Serikali inapanga kujenga bwawa kubwa la maji litakalogharimu takribani Sh24 bilioni litakapokamilika.

Serikali ilikuwa imewaahidi kuwalipa wakazi hao fidia ili wahamie kwingineko na kutoa nafasi ya bwawa hilo kujengwa haraka iwezekanavyo.

Mradi huo ambao ni wa kipekee unajengwa na Wachina.

Hata hivyo tayari familia 150 zimepokea fidia huku wengine wakitarajia kulipwa hivi karibuni.

Bw Peter Ndung’ u, mkazi wa kijiji cha Gathanji, Gatundu Kaskazini, alisema yeye hajapata hata senti moja na anatarajia kulipwa mara moja.

“Sisi kama wakazi wa eneo hilo hatuelewi ni mbinu gani wanatumia kuwafidia wakazi. Wengi wetu bado tunangoja kulipwa haki yetu ili tuweze kujitafutia vipande vya ardhi mahali pengine,” alisema Bw Ndung’ u.

Mnamo Jumamosi iliyopita kulikuwa na uvumi ya kwamba wakazi ambao hawajahama wangefurushwa na maafisa wa GSU kutoka makazi yao ili mradi huo uweze kung’oa nanga.

Bw Peter Ndung’u wa kijiji cha Gathanje. Alisema hajapokea fedha za fidia kupisha ujenzi wa mradi wa Kariminu. Picha/ Lawrence Ongaro

Jumatatu wakazi wengi walikuwa wamengoja hao maafisa wa polisi, lakini hawakuonakana kule.

Uvumi wa Polisi wa GSU kuvamia eneo hilo uliwafanya wakazi wengi kukosa kufanya shughuli zao za kawaida.

Hata hivyo, Bw Mathew Mukuha Mwangi ambaye ni mkazi wa Gathanje alikiri kuwa amepokea fidia ambapo tayari ameihamisha familia yake katika kijiji cha Buchana na kuwajengea nyumba.

“Ninafurahi kupata ya kwamba wazazi wangu wana makao mazuri sasa. Ningewashauri wale wengine waliolipwa kuwa makini na kutumia fedha hizo vyema kabisa,” alisema Mhandisi Mwangi.

Aliiomba serikali kuhakikisha kwamba kila mmoja aliyekuwa apate pesa hizo amelipwa haraka iwezekanavyo.

“Wakazi wengi walitarajia kupokea fedha hizo lakini wakazungushwa kila mara katika benki. Wakati mwingine fedha ziliwekwa kwa akaunti za wakazi hao lakini bado walisumbuliwa kutoa stakabadhi tofauti; jambo lililiwatatiza sana,” alisema Bw Mwangi.

Aliiomba serikali ifanye haraka kuona ya kwamba kila mkazi anayehusika anapokea haki yake bila kuchelewa.

“Wakazi wengine wakienda benki hukosa kuelewa jinsi mambo yanavyoendeshwa. Kwa hivyo serikali ifanye hima iwape mwelekeo jinsi ya kupokea fedha zao za fidia,” alisema Bw Mwangi.

You can share this post!

SWAGG: Don Cheadle

Sabina Chege alenga sheria za kuwapa kina mama wanyonyeshao...

adminleo