Wanakamari wadaiwa Sh26 bilioni na serikali
Na BERNARDINE MUTANU
KAMPUNI za kamari zinadaiwa na serikali Sh26 bilioni, ambazo ni ushuru kwa biashara zao.
Habari hii ni kwa mujibu wa Waziri wa Usalama wa Ndani, Fred Matiang’i, wakati ambapo sekta hiyo inashuhudia misukosuko.
Waziri huyo alilalamika kuwa kampuni za uchezeshaji kamari zinatumia mahakama kutatiza juhudi za Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru (KRA) kuokota mapato hayo.
Serikali hivi majuzi iliagiza kampuni hizo kuomba leseni upya kuanzia Julai 1, katika hatua inalenga kampuni ambazo zimekuwa zikiepuka kulipa ushuru licha ya kupata mabilioni kama faida.
“Yeyote aliyoomba leseni tofauti na hivi sasa anachezesha kamari, niko tayari kutia sahihi nyaraka za kuondolewa nchini leo,” alisema Dkt Matiang’i Jumatatu.
Alitoa agizo hilo siku ambayo Mahakama Kuu iliagiza kusimamisha utekelezaji wa agizo la kudhibiti matangazo ya uchezaji kamari katika vyombo vya habari na utumiaji wa watu maarufu katika matangazo ya mabango.
Marufuku ya utangazaji wa uchezaji wa kamari yalitolewa na Bodi ya Kutoa Leseni na Kudhibiti Uchezaji Kamari (BCLB) kwa lengo la kudhibiti uraibu wa mchezo huo miongoni mwa Wakenya, hasa vijana.
Jaji James Makau alitoa agizo hilo baada ya msanii kuwasilisha kortini kesi ya kupinga agizo hilo, kwa kusema kuwa pato lake na wengine kama yeye lingetatizwa na agizo hilo.