• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Agnettah Zaddock: Anawezaje kuwa mwigizaji hodari na pia mfugaji kuku?

Agnettah Zaddock: Anawezaje kuwa mwigizaji hodari na pia mfugaji kuku?

Na JOHN KIMWERE

AKIWA mdogo alitamani sana kuhitimu kuwa mwanasheria tajika humu nchini. Hata hivyo akiwa sekondari alivutiwa zaidi na masuala ya maigizo taaluma aliyoigeukia baada ya kumaliza shule.

Agnettah Zaddock anayendelea kupalilia kipaji chake huku akiwazia zaidi kushinda tuzo kadhaa katika masuala ya uigizaji. Binti huyu ni mwigizaji pia hufuga kuku wa mayai na nyama mtaani Lucky Summer Kaunti ya Nairobi.

Anasema alianza kufuga kuku mwaka uliyopita biashara anayotarajia angalau kumpiga jeki kimaisha.

”Natamani sana kuibuka mwigizaji mahiri nchini na kushiriki filamu za hadhi ya kimataifa miaka ijayo,” alisema na kuongeza kuwa pia anataka kuwa mwelekezi wa filamu ili kupata nafasi nzuri kuwashika mikono waigizaji chipukizi.

Aidha anasema ”Nataka kufikia levo ya kimataifa ikiwezekana nimpiku staa wa maigizo mzawa wa Marekani Taraji P Henson aliyejipatia umaarufu kutokana na filamu ya Empire.”

Anaongeza kwamba anatamani kufanya kazi na staa huyo. Veterani huyo pia ameshiriki filamu kama ‘What men want,’ ‘Tyler Perry’s Acrimony,’ ‘Hidden figures,’ na ‘The best of enemies,’ kati ya zinginezo.

Agenttah ambaye alianza kushiriki uigizaji na kundi la Pambazuka Arts Quality Production anajivunia kushiriki filamu kadhaa ambazo hupeperushwa kupitia Maisha magic East DStv kama Arnold and Bundi chini ya Insignia Production.

Anawashauri kuwa tayari kukosolewa ili kujiongezea maarifa kuhusu masuala ya uigizaji. Picha/ John Kimwere

Pia aliwahi kufanya kazi na makundi mengine kama ‘Fanaka Arts,’ ‘Jawabu Production,’ na ‘Shangilia Theatre.’

Mwigizaji huyu hufanya kazi na kundi la Son of Man International alilojiunga nalo mwaka jana. Katika kundi hilo anajivunia kushiriki filamu kadhaa tangu Desemba mwaka uliyopita ikiwamo ‘Maria Joseph,’ Maxwell Easter,’ na Maxwell Christmas bila kusahau ‘The lady with Red,’ kati ya zingine.

Anashauri wasanii chipukizi kuwa hakuna kizuri huja rahisi lazima wasake riziki kwa kujituma mithili ya mchwa na kujiaminia wanaweza. Pia anawaambia kwamba nyakati zote wakipata nafasi ya kuigiza wanastahili kujitolea mhanga na kufanya kazi kadiri ya uwezo wao ili kuvutia wahusika.

Chipukizi huyu anashikilia kwamba sekta ya maigizo nchini tayari inaonyesha dalili za kupiga hatua. Lakini anadai serikali ya kitaifa inastahili kuwekeza zaidi katika tasnia ya uigizaji ili kutoa nafasi za ajira kwa wasanii chipukizi.

Je, msanii huyu amekumbana na changamoto gani? Mwigizaji huyu mwenye umri wa miaka 31 anasema imekuwa vigumu kushawishi familia yake kwamba sanaa inalipa maana imekuwa mstari wa mbele kumpiga.

”Wanafamilia yangu wanaamini sanaa siyo ajira nzuri kamwe haiwezi kutegemewa,” alisema na kuongeza kuwa malipo duni huwavunja moyo wengi wao pia kufanya kazi katika mazingira magumu.

You can share this post!

Washiriki wapya Super 8 watisha wakali wa soka

Mwanamke amuua mumewe kwa kumuuliza sababu ya kuwa mlevi

adminleo