• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 6:55 AM
Raila akamilisha ziara ya mataifa ya DRC, Niger na Ghana

Raila akamilisha ziara ya mataifa ya DRC, Niger na Ghana

Na CHARLES WASONGA

MJUMBE wa Umoja wa Afrika (AU) kuhusu miundo msingi Raila Odinga amekamilisha ziara ya siku tatu ya kujadili ajenda ya miundombinu na viongozi kadha wa Afrika.

Alifanya mkutano huo mwezi mmoja kabla ya kuandaliwa kwa Kongamano Maalum la Marais wa Mataifa wanachama wa AU mnamo Julai nchini Niger.

Mwishoni wiki Bw Odinga alifanya mazungumzo na Rais Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ambapo walijadili mpango wa ujenzi wa daraja la Kinshasa-Brazzaville ambalo liko katika barabara kuu ya Tripoli kwenda Cape Town.

Msemaji wa Bw Odinga Denis Onyango, kwenye taarifa alisema viongozi hao wawili pia wakijadili hatua ambazo zimepigwa katika ujenzi wa bwawa la Inga katika mto Congo. Mradi huo ukitekelezwa utakuwa mradi mkubwa zaidi wa uzalishaji wa kawi barani Afrika.

Kutoka Kinshasa, Bw Odinga alisafiri hadi jijini Niamey, Niger kufanya mazungumzo na Rais Mahamadou Issoufou ambaye ni mtetezi sugu wa mkataba wa Biashara huru Afrika African Continental Free Trade Area (ACFTA) iliyotiwa saini mnamo 2018.

Mkataba huo utaanza kufanya kazi baada ya kuidhinishwa na mataifa 50.

Bw Odinga alimweleza Rais Issoufou kuhusu mpango wa ujenzi wa Barabara Kuu ya Afrika na ajenda nzima ya miundo msingi ikiwemo reli na safari za ndege huku akisitiza umuhimu wayo.

Viongozi hao wawili waliafikiana kufanya majadiliano ya pembeni wakati wa Kongamano la Marais wa Mataifa ya Wachama wa AU nchini Niger Julai.

Bw Odinga alikamilisha ziara yake kufanya mkutano na Rais Nana Akufo-Addo wa Ghana. Alimpasha Rais huyo kuhusu ajenda ya AU kuhusu miundo msingi huku akimtaka kuunga mkono.

Kiongozi wa ODM anarejea nchini wakati ambapo jina lake na la Rais Uhuru Kenyatta yanatajwa katika sakata ya usafirishaji wa dhahabu feki hadi Dubai.

Jina la Odinga lilitajwa katika kanda ya sauti ambapo inadaiwa kuwa aliahidi kuingilia kati ili kuwezesha dhahabu hiyo kufirishwa hadi Muungano wa Milki ya Kiarabu (UAE).

You can share this post!

Kenya yaapa kutojadiliana na Al Shabaab

DHAHABU FEKI: Washukiwa ndani hadi Juni 27

adminleo