2022: Nalengwa katika mbio za Ikulu – Waiguru
Na PAUL WAFULA
GAVANA wa Kirinyaga, Bi Anne Waiguru amedai kuna wanasiasa wawili wakuu ambao wanamnyemelea wakitaka awe mgombea mwenza wao kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.
Bi Waiguru, anayehudumu kipindi cha kwanza cha ugavana, alisema kwa sasa hajafanya uamuzi kuhusu mapendekezo hayo, lakini atatangaza hatua atakayochukua wakati unaostahili.
“Nimepokea maombi mawili ya wadhifa wa Naibu Rais, lakini huu sio wakati mwafaka wa kuwataja wanaotaka niwe mgombea mwenza,” alisema kwenye mahojiano ya kipekee na Taifa Leo.
Kufikia sasa, wadadisi wa kisiasa wanaonelea kwamba ushindani wa urais 2022 utakuwa zaidi kati ya Naibu Rais William Ruto na Kiongozi wa Chama cha ODM, Raila Odinga, ambaye bado hajaweka wazi iwapo atawania tena wadhifa huo.
Ingawa Bi Waiguru alikataa kutaja majina ya wanaomnyemelea, alisema anaamini Chama cha Jubilee ndicho kitaunda serikali ijayo, na anatarajia kutekeleza wajibu muhimu kisiasa katika eneo la Mlima Kenya, lililo na wapigakura wengi ili chama hicho kipate ushindi.
Dkt Ruto anaendelea kupigiwa debe kuwa mgombea urais wa Jubilee, lakini kuna kikundi kingine cha wanasiasa katika chama hicho kinachompinga.
Bi Waiguru, ambaye pia ni naibu mwenyekiti wa Baraza la Magavana (CoG), anasema eneo la Mlima Kenya sharti liwe katika serikali ijayo na hilo ndilo litakuwa jukumu lake wakati kinyang’anyiro cha kumrithi Rais Kenyatta kitakapoanza rasmi.
“Naona jukumu langu litakuwa ni kuhakikisha kwamba kaunti 10 za eneo la Mlima Kenya zitapata haki yake katika serikali ijayo. Hatutaki viongozi watakaoteuliwa kwa siri eneo hili bali mtu ambaye atachaguliwa na wananchi,” alisema.
Viongozi kadhaa wa Mlima Kenya wamekuwa wakitaka kuwa wagombea wenza kwenye uchaguzi mkuu wa 2022 baada ya kipindi cha Rais Kenyatta kukamilika. Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria ametangaza kuwa atagombea urais kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.
Wengine wanaotaka kuongoza eneo hilo ni aliyekuwa mgombea urais Peter Kenneth, Gavana wa Murang’a Mwangi wa Iria, Seneta wa Tharaka Nithi Kithure Kindiki, Gavana wa Meru Kiraitu Murungi na aliyekuwa gavana wa Kiambu William Kabogo.
Gavana huyo alijitenga na kundi linalodai eneo hilo halijafaidika kikamilifu na miradi ya maendeleo akisema hayo ni maoni ya watu wachache.
Alisema japo kuna tatizo la sera linalopaswa kushughulikiwa ili kuhakikisha eneo hilo halinyimwi haki, linapata miradi mingi katika bajeti ya kitaifa.
Kuhusu suala la kura ya maamuzi, Bi Waiguru alisema mageuzi yanafaa ili kulainisha uongozi katika taifa.
“Kura ya maamuzi inafaa ili kutatua suala la uongozi wa kitaifa. Tulidhani mfumo wa utawala wa urais ungesuluhisha masuala haya ya uwakilishi, lakini hili halijatendeka. Hii ndiyo sababu ya haja ya kupanua nafasi katika ngazi ya juu ili watu wahisi wamewakilishwa,” akasema.
Kulingana naye, serikali za kaunti pia zinapasa kujitetea ili zitengewe pesa zaidi kutoka asilimia 15 hadi asilimia 40 ya bajeti ya kitaifa.