Habari Mseto

Ndani kwa kumuua mwenzake wakizozania aliyeshinda kamari

May 22nd, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na PETER MBURU

MWANAMUME kutoka Murang’a ambaye alishtakiwa kwa kumuua rafiki yake kufuatia mzozo wa mamari amefungwa miaka mitatu jela na mahakama moja, baada ya kupatikana na hatia.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Murang’a Kanyi Kimondo alikuwa amemfunga Ibrahim Mugera miaka kumi gerezani kwa kumuua marehemu Joseph Gitau, lakini akabadili uamuzi wake kutokana na muda ambao mshtakiwa amekuwa kizuizini.

Kupitia wakili wake, Bw Mugera aliiomba korti kumhurumia kwa kuwa ilikuwa mara ya kwanza kufanya kosa la aina hiyo, akisema hakulenga kumuua rafikiye.

Lakini jaji huyo alisema kuwa kutokana na matendo yake, maisha ya mtu asiye na makosa yalipotezwa, kwa kisa kidogo ambacho kingesuluhishwa.

Mshtakiwa alimdunga rafikiye kisu walipokuwa nyumbani kwao Kandara mnamo 2010, walipozozana kuhusu nani alikuwa ameshinda kamari.

Bw Gitau alifariki alipokuwa akikimbizwa hospitalini.

“Sharti mshtakiwa awajibike kwa maisha ambayo yalipotezwa. Korti inaamua kuwa kifungo cha nje hakifai,” akasema Jaji.