Waziri ashtuka kuwekewa ndumba afisini mwake
Na STEPHEN ODUOR
TETESI za maafisa wa serikali ya Kaunti ya Tana River kuroga wenzao, zimeibuka baada ya waziri katika kaunti hiyo kupata amewekewa ndumba za kichawi afisini mwake.
Kulingana na afisa wa ngazi za juu katika serikali hiyo aliyeomba kubanwa jina, waziri huyo alifika afisini mwake ambapo alifaa kuwa na mkutano wa dharura lakini alipofungua mlango, alipata vikorokoro kadhaa mezani mwake.
Kwa mshtuko aliwaita wadogo wake na watu waliokuwa karibu kushuhudia kilichokuwemo afisini, huku jasho jebamba likimtoka usoni.
Ilichukua muda kuweza kubaini jinsi vifaa hivyo vya kichawi viliingizwa hadi mezani mwake, na hivyo kuwapelekea kuchunguza kwa kurejelea kamera za CCTV.
Hata hivyo, matokeo ya uchunguzi huo hayakufichuliwa kwa umma, huku duru zikisema inashukiwa mhusika ni mmoja wa watumishi wenzake ambaye walikuwa wamekosana awali.
Habari zilieleza kuwa adui huyo wake amekuwa akimlaumu waziri msimamizi wa idara hiyo kwa masaibu yake ya kuandamwa na madai ya ufisadi, huku akisikika kumtaja waziri huyo kwenye vikao akimlaumu kwa kumchongea kikazi.
Duru za kuaminika zinasema kuwa wawili hao hawajakuwa wakiongea kwa muda, tangu waziri alipowasilisha ripoti katika afisi ya gavana kuhusu wizi wa pesa katika idara hiyo, ripoti inayotishia kummwagia unga hasimu huyo wa waziri.
Mvutano umekuwepo kwa muda kati ya baadhi ya mawaziri na maafisa wengine wa serikali ya kaunti hiyo.