IEBC yasema inahitaji Sh8 bilioni kutathmini upya mipaka
Na BERNARDINE MUTANU
Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka nchini (IEBC) inahitaji Sh8 bilioni kutathmini mipaka ya maeneobunge na wadi kwa mara ya pili.
Kulingana na mwenyekiti wa IEBC Bw Wafula Chebukati, tathmini inafaa kufanyika kati ya Februari na Agosti 3, 2021.
Alisema hayo alipofika mbele ya Kamati ya Bunge kuhusu Utekelezaji wa Katiba inayosimamiwa na Bw Jeremiah Kioni, Mbunge wa Ndaragwa.
Kulingana na Bw Chebukati, watategemea data kutoka kwa ripoti kuhusu idadi ya watu nchini inayotarajiwa kutolewa mwaka 2019.
Kulingana na kifungu cha 89 cha Katiba, IEBC inafaa kutathmini mipaka kati ya miaka nane na miaka 12 na tathmini inafaa kukamilika mwaka mmoja kabla ya uchaguzi wa ubunge kufanywa.
Itakuwa tathmini ya kwanza tangu Katiba mpya kuzinduliwa 2010. Mipaka ya maeneobunge na wadi iliundwa kwa kufuata katiba hiyo.