Habari Mseto

Ujumbe wa Central Youth 4Ruto 2022 kwa wapinzani wao eneo la Mlima Kenya

May 23rd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MWANGI MUIRURI

VUGUVUGU la vijana Mlima Kenya linalompigia debe Naibu Rais William Ruto kurithi urais baada ya uchaguzi mkuu wa 2022 sasa linawataka wanasiasa wanaopingana nao eneo hilo waandae mikutano yao hadharani.

Vuguvugu hilo likijifahamisha kama ‘Central Youth 4Ruto 2022’ chini ya ukatibu wa Dishon Warui na mwenyekiti Samuel Maina limesema kuwa wanasiasa hao wanafaa waandalie Wakenya ushahidi tosha kuwa “mito yao ya kupinga Ruto inachukuliwa kwa makini Mlima Kenya.”

Akasema Bw Warui kwa Taifa Leo katika mahojiano ya moja kwa moja: “Ningewataka wabunge Maina Kamanda (maalumu), Gathoni wa Muchomba (Mwakilishi wa Wanawake wa Kaunti ya Kiambu katika Bunge la Kitaifa), mbunge wa Nyeri Mjini Wambugu Nyamu na wengine walioanguka kura kama Jamleck Kamau,  Elias Mbau na Joshua Toro watangaze mkutano wa hadhara katika uwanja wowote Mlima Kenya.

“Tuwajuavyo, kazi yao ni kuandaa mikutano katika maeneo ya Kibra jijini Nairobi, katika mikahawa na kwa vituo vya redio na magazeti wakidai kuwa Mlima Kenya una kura zote zikikaidi Dkt Ruto. Waje katika mkutano wa hadhara katika uwanja wowote wa umma Mlima Kenya na watangaze hayo runinga zikipeperusha ushahidi wao moja kwa moja,” akasema.

Bw Maina aliteta kuwa “hawa wanasiasa kile walijaliwa kwa wingi ni ubinafsi wa kujitafutia makuu na ambapo wanatumia jina la Mlima Kenya kama chambo cha kujikusanyia manufaa.”

Amewataka walio ndani ya ukaidi wa Dkt Ruto Mlima Kenya watangaze waziwazi ni nani wanaunga mkono.

“Tunajua mshindani mkuu wa Dkt Ruto 2022 atakuwa ni Raila Odinga. Unaposema hutambui uwaniaji wa Dkt Ruto, unafaa utuambie basi tumuunge mkono nani. Hawasemi wanaunga mkono Ruto na hawasemi wanamuunga mkono Raila au mwingine katika ushindani. Hawa ni watu ambao wamechanganyikiwa na kazi yao ni kuandaa tu vita vya kimaneno bila kuwa na ulainifu wa mikakati ya wako wapi kisiasa,” akasema.

Alisema wafuasi wa Ruto eneo la Mlima Kenya wamekuwa wakiandaa mikutano mashinani kila ikibidi “na huwa mnatuona tukiwa na wafuasi wapigakura wetu tukitangamana bila wasiwasi wowote.”

Lakini, akahoji: “Huwa hatuelewi ni kwa nini ninyi huwaogopa wapigakura hawa kwa kuwa hatuwaoni mkitangamana nao licha ya kuwa kila siku mnatuambia wapigakura hao hawako na Ruto.”