Habari Mseto

Shehe kusalia ndani kuhusu ugaidi

February 21st, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Sheikh Guyo Gorsa Boru akiwa kizimbani katika Mahakama ya Milimani Februari 20, 2018 aliposhtakiwa kuwa mwanachama wa Al Shabaab. Picha/ Maktaba

Na RICHARD MUNGUTI

MHUBIRI wa Kiislamu  mashuhuri mjini Marsabit atakaa gerezani hadi kesi ya ugaidi dhidi yake itakapoamuliwa.

 Sheikh Guyo Gorsa Boru ambaye kukamatwa kwake mjini Marsabit Januari 13 kulisababisha ghasia zilizopelekea kuuawa kwa mtu mmoja na magari ya polisi kuchomwa, amezuiliwa katika gereza la Kamiti

Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP), alimsihi hakimu mkuu Francis Andayi aamuru Sheikh Boru azuiliwe kwa vile atavuruga mashahidi.

Alishtakiwa kuwa mwanachama wa  kundi la kigaidi la Al Shabaab lililopigwa marufuku na serikali.

“Polisi wanataka kumhoji mshukiwa huyu anayependwa sana mjini Marsabit kuhusu mafunzo ya itikadi kali  kwa vijana na ushirika wake katika Al Shabaab walioko nchini Somalia,” alisema kiongozi wa mashtaka, Bw Duncan Ondimu Jumanne.