DP Ruto ataka wafanyabiashara wadogowadogo wapigwe jeki ya asilimia 60
Na MWANGI MUIRURI
NAIBU wa Rais Dkt William Ruto amewataka mawaziri wa kilimo na viwanda na biashara wawajibikie suala la wafanyabiashara wa Kenya kusukumwa nje ya soko lao na upenyo wa biashara huru katika jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Akizungumza Alhamisi katika kituo cha redio na TV cha Kameme, aliwataka mawaziri hao ambao ni Mwangi Kiunjuri na Peter Munya wahakikishe kuwa kumewekwa sera maalum za kuwapiga wakulima wa Kenya jeki ya uzalishaji kwa asilimia 40 nayo gharama ya ushuru imepunguka kwa takriban asilimia 20.
“Gharama ya uzalishaji sambamba na ile ya kiushuru ndiyo huchangia bei. Utafiti umeonyesha kuwa mataifa majirani zetu ambayo yanatuhangaisha hapa sokoni yamepiga jeki wakulima wao katika safu hizo mbili muhimu,” akasema.
Kwa mfano, Dkt Ruto alisema kuwa mahindi ambayo huchangia asilimia kubwa ya chakula ya mifugo huwa na bei ya chini katika mataifa hayo.
“Unapata kuwa hapa nchini gunia hilo hapa Kenya linagharimu Sh3,000 na zaidi. Nchini Uganda gunia hilo ni Sh900. Hapo ndipo shida kubwa iko katika hitilafu ya ushindani wa bei hapa nchini,” akasema.
Alisema kuwa wakulima ndio wameumia zaidi katika soko hilo, akitaja wafugaji wa kuku wa mayai, maziwa na mboga na matunda kama waathiriwa ambao wanatazamia sera za dharura za kuwakinga.
“Nimeongea na Kiunjuri na nimemwambia ajue sisi kama wakulima na wafanyabiashara wa Kenya tunaumia katika soko mikononi mwa wafanyabiashara wa mataifa jirani. Nimeongea naye kama Naibu Rais na pia kama mkulima ambaye kwa mfano anaumia katika soko la mayai…Mimi ni mfugaji wa kuku wa mayai,” akasema.
Dkt Ruto alisema kuwa mayai kutoka taifa la Uganda kwa mfano yanauzwa kwa kila moja kwa Sh7 huku mfugaji wa Kenya aking’ang’ania bei ya Sh10 kwa kila moja.
“Hilo lina maana kuwa tofauto hiyo ya bei inawatuma wateja kwa vibanda vya hawa wageni kujipa mayai…Swali ambalo tunamtaka Kiunjuri ajibu ni kuhusu uhalali wa bei hiyo ya Uganda na pia ni kwa msingi gani imewezekana kuwa ya chini kiwango hicho,” akasema Ruto.
Aidha, alisema kuwa sera zote za kibiashara hasa zile za uagizaji bidhaa kutoka ng’ambo zinafaa kuwekwa katika viwango vya utoshelevu wa wafanyabiashara wadogowadogo.
“Waziri wa biashara alipewa idhini ya kulegeza masharti makali ambayo yamewekwa dhidi ya waagizaji bidhaa katika vita dhidi ya bidhaa ghusi na visivyozingatia ubora… Hili litumike kuwakinga wafanyabiashara wadogowadogo kutokana na uhasi wa sheria hizo,” akasema.