Wimbi lazuka vyama vingine 4 vikitaka usajili
Na KAMAU WANDERI Na CHARLES WASONGA
VYAMA vingine vinne vya kisiasa vimewasilisha maombi vikitaka visajiliwe rasmi huku wimbi la kuchipuka kwa vyama vipya likiendelea kuvuma nchini, msajili wa vyama vya kisiasa Ann Nderitu amesema.
Kwenye tangazo katika gazeti rasmi la serikali toleo la Ijumaa Bi Nderitu alisema vyama hivyo ni; Party of Economic Democracy (PED), National Reconstruction Alliance (NRA), Unified Change Party (UCP), Ushirika wa Haki na Maendeleo.
“Kulingana na mamlaka yaliyoko katika kipengee cha 5 (2) cha Sheria ya Vyama vya Kisiasa ya 2011, afisi ya msajili wa vyama vya kisiasa inatoa ilani kwamba vyama vilivyotajwa katika tangazo hili vimewasilisha ombi la kutaka kupewa usajili wa muda kulingana na kipengee cha 5 na 6,” akasema Bi Nderitu.
Nembo ya chama cha PED ni mchoro wa watu wanaopanda ngazi huku rangi zake zikiwa kijani kibichi, nyekundu na nyeusi huku NRA ikiwa na nembo ya ndege aina ya tai na rangi zake zikiwa samawati na nyekundu.
Na nembo ya chama cha UCP ni mduara wenye rangi ya samawati na herufi ya jina lake huku rangi zake zikiwa samawati na nyeupe huku kile cha UHM kikiwa kimeteua tufe (mpira) kama nembo yake na rangi za samawati, nyeupe na nyeusi.
“Yeyote mwenye pingamizi kuhusu usajili wa vyama hivyo anaombwa kuiwasilisha, kwa maandishi, kwa Msajili wa Vyama vya Kisiasa ndani ya siku saba,” akasema Bi Nderitu.
Idadi ya vyama vya kisiasa nchini itatimu 68 endapo usajili wa vyama hivi vinne utakubaliwa.
The Transformation National Alliance Party (TNAP) ndicho chama cha hivi punde kusajiliwa.
Chama hiki kinachohusishwa na Mbunge wa Gatundu Kusini kilibuniwa na baadhi ya wanachama wa Jubilee ambao waliingiwa na hofu kuhusu dalili za kusambaratika kwa chama hicho tawala.
Hii ni kufuatia kuchipuza kwa makundi ya “Kieleweke” kinachopinga azma ya Naibu Rais William Ruto kuwania urais 2022, na “Team Tangatanga” kinachompigia debe Dkt Ruto kama anayefaa kumrithi Rais Uhuru Kenyatta atakapostaafu. Wakati huo huo, chama cha Transformation National Alliance (TNAP), kimebadilisha nembo yake kufuatia agizo kutoka kwa Msajili Mkuu wa Vyama vya Kisiasa, Bi Anne Nderitu.
Noti za pesa
Chama hicho sasa kitakuwa na noti za pesa kama nembo yake mpya, kinyume na awali, ambapo nembo yake ilikuwa njiwa mwenye rangi nyekundu na samawati.
Muda mfupi baada ya kusajiliwa mnamo Mei 6, Bi Nderitu aliwataka maafisa wakuu wa chama hicho kubadili nembo na jina lake, kwani zilikuwa zikiwiana na chama cha The National Alliance (TNA) kilichokuwa kikiongozwa na Rais Uhuru Kenyatta.
TNA ilivunjwa baada ya kuungana na URP kati ya vyama vingine kubuni Chama cha Jubilee (JP) mnamo 2017.
Lakini kwenye barua alichokiandikia mnamo Jumatano, msajili huyo alieleza kuridhishwa na mabadiliko ya nembo na ufupisho wake.
Badala ya kujiita TNA, ufupisho wake utakuwa TNAP.
“Tumekubali nembo mpya mliyopendekeza, baada ya kuzingatia sheria na kanuni za usajili wa vyama. Mnaagizwa kuwasilisha nembo hizo rasmi kwa afisi yangu,” ikasema barua hiyo.
Hata hivyo, kaulimbiu ya chama hicho, ambacho kinahusishwa na mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria haikubadilika. Kaulimbiu yake ni: ‘Kazi na Pesa.’