JAMVI: Wanasiasa wakongwe Mlima Kenya waanza kujifufua wakilenga 2022
Na WANDERI KAMAU
WANASIASA wakongwe katika ukanda wa Mlima Kenya wameanza kutumia mawimbi yaliyopo kujifufua kisiasa, huku wengi wakionekana kujitayarisha kuwania nyadhifa mbalimbali kwenye uchaguzi wa 2022.
Baadhi yao wamekuwa wakiandamana na makundi ya wazee katika hafla mbalimbali, huku wadadisi wakisema kuwa lengo lao ni kufufua nyota zao kadiri mwaka 2022 unavyozidi kukaribia.
Baadhi ya wanasiasa ambao wamejitokeza wazi ni mbunge maalum Maina Kamanda, aliyekuwa mbunge wa Molo, Njenga Mungai, mbunge wa zamani wa Limuru, George Nyanja, mbunge wa zamani wa Subukia Koigi wa Wamwere, mbunge wa zamani wa Gachoka Joseph Nyaga, waziri wa zamani Kirugi M’Mukindia kati ya wengine wengi.
Wanasiasa hao walihudumu katika miaka ya themanini na tisini, ambapo wadadisi wanasema wanatumia ushawishi wao wa kisiasa kutafuta upenyu katika uchaguzi ujao.
Bw Kamanda, ambaye alihudumu kwa miaka mingi kama mbunge wa Starehe na Waziri wa Serikali za Mitaa, amejitokeza kama mtetezi mkuu wa Rais Uhuru Kenyatta kupitia mrengo wa ‘Kieleweke.’
Bw Kamanda ameibukia kuwa sauti kuu katika kundi hilo ambalo linapinga azma ya Naibu Rais William Ruto kuwania urais mnamo 2022.
Kundi hilo limekuwa likisisitiza kwamba lazima Dkt Ruto na kundi la ‘Tanga Tanga’ limheshimu Rais Kenyatta kwa kuunga mkono vita anavyoendesha dhidi ya ufisadi.
Lakini kulingana na wachanganuzi wa masuala ya kisiasa, kujitokeza kwa Bw Kamanda kama mtetezi wa Rais Kenyatta ni mkakati anaotumia kuhakikisha kuwa amejiweka katika nafasi atakapotambulika na wengi pindi atakapotangaza azma ya kuwania nafasi yoyote ya kisiasa mnamo 2022.
“Bw Kamanda ni mwanasiasa ambaye ana tajriba kubwa sana. Anafahamu kwamba lazima ajiweke katika nafasi ambayo itakuwa rahisi kukubalika na watu atakapotangaza azma ya kuwania nafasi yoyote; iwe ni ubunge, ugavana ama useneta,” asema Kiprotich Mutai, ambaye ni mchanganuzi wa kisiasa.
Bw Kamanda aliteuliwa na Chama cha Jubilee (JP) kuwa mbunge maalum ili kutatua mzozo ulioibuka kwenye shughuli za mchujo katika eneobunge hilo kati yake na mbunge wa sasa, Charles Njagua.
Wikendi iliyopita, Bw Mungai aliongoza ujumbe wa wazee na akina mama kutoka Kaunti ya Nakuru kumtembelea kiongozi wa ODM, Raila Odinga, katika makazi yake ya eneo la Opoda, Kaunti ya Kisumu.
Kwenye ziara hiyo, Bw Mungai alisisitiza kwamba jamii za GEMA (Agikuyu, Aembu na Ameru) zitamuunga mkono ikiwa atatangaza kuwania urais mnamo 2022.
Wazungumzaji wengine walisisitiza kuwa jamii hiyo (hasa Wakikuyu wanaoishi katika ukanda wa Bonde la Ufa) watamuunga mkono Bw Odinga bila shinikizo zozote.
Kulingana na wachanganuzi, lengo la Bw Mungai ni kutumia mzozo wa kisiasa uliopo kati ya Dkt Ruto na Bw Odinga katika udhibiti wa kisiasa wa eneo hilo kujijenga.
“Huyu ni mwanasiasa anayefahamu atajipatia umaarufu mkubwa kwa kuyaingiza majina ya Dkt Ruto na Bw Odinga kwenye mkakati wa kujifufua kisiasa,” asema Prof Macharia Munene.
Kulingana na Prof Munene, wanasiasa zaidi wataendelea kujitokeza, kwani wengi wao wanatamani nyadhifa za sasa za uongozi kwani zina ushawishi mkubwa ikilinganishwa na zamani.
“Wanasiasa wengi wanapania kuwa magavana na maseneta kwani watapata nafasi ya kudhibiti kiwango kikubwa cha fedha ikilinganishwa na zamani. Hivyo, wataendelea kujitokeza na kutumia majukwaa yaliyopo kujinadi kisiasa kwa wananchi,” asema mchanganuzi huyo.
Kulingana na Bw Nyanja, aliyehudumu kama mbunge wa Limuru na kuwania useneta katika Kaunti ya Kiambu mnamo 2017, lengo lao si kuwania nyadhifa mbalimbali tu, lakini pia kutoa ushauri kwa viongozi wengi wachanga.
“Viongozi wengi wa sasa ni wachanga. Hivyo, wanahitaji miongozo yetu kama wanasiasa waliohudumu awali na walio na ufahamu mwingi kuhusu masuala ya uongozi. Hilo ndilo linalotupa msukumo,” asema Bw Nyanja.Kiongozi huyo amekuwa akijihusisha na shughuli mbalimbali za kijamii, lakini ametangaza wazi kuwa anaunga mkono msimamo wa kundi la ‘Kieleweke.’
Kwa upande wake, Bw Wamwere, ambaye amewania useneta katika Kaunti ya Nakuru mara mbili bila kufaulu, amesema kuwa wanasiasa wakongwe wana mchango mkubwa wanaoweza kutoa kwa uongozi wa sasa.
Kulingana na Bw Wamwere, uongozi wa sasa hauwezi kufaulu bila mchango wa watangulizi wao.
“Kuna mchango mkubwa tunaoweza kutoa kwa viongozi wa sasa. Vilevile, tuna ufahamu mkubwa wa historia ya siasa la taifa hili. Hili linamaanisha kuwa wananchi na viongozi wenyewe wanatuhitaji zaidi kuliko vile tunavyowahitaji,” asema Bw Wamwere.
Ingawa hajaeleza wazi ikiwa atawania tena useneta mnamo 2022, Bw Wamwere amekuwa akishiriki katika vipindi mbalimbali vya mijadala ya kisiasa.
Wachanganuzi wanatabiri mchipuko wa makundi zaidi ya wanasiasa, ikizingatiwa kuwa wengi hawakupewa kazi kwenye teuzi zilizofanywa majuzi na Rais Kenyatta.