Makala

Vannesa mwigizaji wa Tahidi High alenga kumfikia Maisie Williams

May 26th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na JOHN KIMWERE

SURA na jina lake siyo geni kwa wapenzi wa tasnia ya filamu hapa nchini. Ni miongoni mwa wasanii wengi wa kike wanaovumisha jukwaa la burudani ya uigizaji huku wakilenga kufikia viwango vya kimataifa miaka ijayo.

Amefanikiwa kuvutia wafuasi wengi tu ambao hufuatilia anavyofanya vionja katika kipindi cha ‘Tahidi High’ ambacho hupeperushwa kupitia Citizen TV kilicho kati ya vipindi maarufu hapa nchini.

Ingawa alivutiwa na uigizaji akisoma darasa la tano, kama taaluma alianza kujituma katika ulingo huu mwaka 2012 baada ya kukamilisha elimu ya sekondari.

Binti Wambui Kibue ambaye katika uhusika wake kisanaa anafahamika kama Vannesa amehitimu kwa shahada ya digrii kuhusu masuala ya uigizaji katika Chuo Kikuu cha Kenyatta(KU).

Kando na uigizaji kipusa huyu ni prodyuza wa kuzalisha filamu pia mwandishi wa script za filamu. ”Ingawa mwanzo nilivutiwa na uigizaji kuna kipindi nilitamani kuhitimu kuwa daktari lakini uigizaji uliyeyusha kabisa matamanio hayo,” alisema na kuongeza kuwa anajivunia kushiriki kazi nyingi tu pengine kinyume na matarajio ya wengine.

Anasema uigizaji ni talanta ipo katika damu yake maana punde baada ya kumaliza shule ya upili alibahatika kuwa miongoni mwa walioshiriki kipindi kilichofahamika kama ‘Makutano Junction’ kilichorushwa kupitia Citizen TV.

Mwigizaji chipikuzi Wambui Kibue almaarufu Vannesa. Picha/ John Kimwere

”Hakuna mwanadamu asiyena malengo katika taaluma yake ambapo mimi nawazia kufikia kiwango cha staa wa maigizo mzawa wa Uingereza, Maisie Williams ambaye hushiriki drama series iitwayo Game of Thrones. Mwigizaji huyu pia ameshiriki filamu kibao ikiwemo ‘Doctor who,’ ‘The Falling,’ na ‘The book of love,’ kati ya zinginezo.

Binti huyu anajivunia kushiriki vipindi mbali mbali zilizowahi kuonyeshwa kupitia runinga tofauti nchini ikiwemo Citizen TV, NTV na KU TV.

Kando na Tahidi High pia Makutano Junction, ameshiriki filamu kama ‘Higher learning,’ ‘Salma,’ bila kusahau michezo ya kuigiza ikiwemo ‘What cant kill you,’ ‘Careless in red,’ na ‘Deliberate Contempt.’

”Kusema kweli bila kujisifia nimefanya kazi nyingi tu katika masuala ya uigizaji,” alisema na kuongeza kuwa amepania kutumia talanta yake kubadilisha maisha ya wengi, kimawazo pia kuelimisha jamii ili iweze kutazama dunia kwa mwamko mpya.

Mwigizaji huyu anasema angependa sana kufanya kazi na wasanii mbali mbali wazalendo wenzake akiwemo Lupita Nyong’o, Pauline Kyalo na Melissa Kiplagat kati ya wengine.

Je demu huyu amepatia changamoto gani? Anasema kuhudhuria majaribio bila kuchukulia ni jambo limewahi fanya avunjike moyo. Aidha analia maprodyuza mafisi ambao hupenda kushusha hadhi ya wanawake kwa kuwataka kimapenzi ili kuwapa ajira.

Binti huyu siyo mchoyo wa mawaidha. Anashauri waigizaji wanaokuja kwamba wanapoigiza wanastahili kuonyesha talanta yao kwa kujitolea na kujiamini wanaweza bila kujishusha. Pia anasema wapaswa kutia bidii na kujipa moyo nyakati zote.