• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 7:45 AM
Madalali wavamia kiwanda cha pareto kupiga mnada magari

Madalali wavamia kiwanda cha pareto kupiga mnada magari

NA RICHARD MAOSI

Madalali Jumamosi walivamia kampuni ya kuzalisha pareto, Kenya Processing Company tawi la Nakuru, wakitaka kupiga mnada magari matatu ambayo yamesalia kuendesha shughuli za kusafirisha pareto kutoka kwa wakulima hadi kiwandani.

Akizungumza na Taifa Leo Dijitali, msimamizi wa wafanyakazi kiwandani humo Bw George Onyango alisema watu saba wasiojulikana walivamia kiwanda wakitaka kuchukua magari hayo.

“Waliingia kama wahalifu kisha wakavunja kufuli kwenye lango kuu baada ya kuzozana na walinzi waliokuwa wameshika doria,” Bw Onyango akasema.

Ingawa magari hayo ni kuukuu walishikilia kuwa ni lazima waondoke nayo,wakidai kampuni ilikuwa na deni kubwa ambayo serikali haikuwa imelipa.

Onyango anasema walianzisha vurugu pale walinzi walipoomba wajitambulishe kwa kutoa vitambulisho au agizo la korti au stakabadhi nyinginezo lakini walikataa.

“Lakini baadaye walilegeza msimamo wakisema walikuwa ni maafisa wa usalama waliotumwa na madali ili wasaidie kwenye shughuli za kupiga mali ya kampuni mnada,”alisema.

Onyango alisema madali hao wangeondoka na magari hayo matatu endapo sio wafanyikazi waliojitokeza kwa wakati kuwakabili.

Wafanyakazi wa kampuni hiyo walitazama kwa umbali. Picha/ Richard Maosi

Aidha, madali hao walikataa kuzungumza na wanahabari na muda kidogo baadaye wakatimua mbio walipoona kamera.

“Mwaka uliopita dalali mwingine alipata kibali kutoka kwenye mahakama,akachukua magari manne kati ya saba na haya matatu yaliyobaki ndiyo tegemeo letu,” Bw Onyango aliongezea.

Mnamo 2018 gavana wa Nakuru Lee Kinyanjui aliwaomba washikadau kuungana na serikali ya kaunti katika juhudi za kufufua kilimo cha pareto katika kaunti 18 .

Katika nchi ya Kenya ni zaidi ya kaunti 20 zinazoendesha kilimo hiki cha pareto West Pokot ikiongoza kwa uzalishaji wa pareto ya hali ya juu.

Lee aliongezea kuwa mbali ya viwanda kudidimia nchini,zao la pareto nchini lilikuwa limepoteza mashiko yake kwenye soko la kimataifa.

Lee alisema uongozi wake umeweka mikakati ya kuhakikisha kiwanda cha pareto kinarudia hadhi yake ya zamani,ikizingatiwa kuwa wakulima wadogo walikuwa wakipata kupata soko la mazao .

Wengi wao walikuwa wamegeukia kilimo mbadala kama vile ukuzaji wa mahindi, baada ya kukadiria hasara kubwa mazao yakiozea shambani.

Pia vijana wengi walikuwa wakihangaika kutokana na ukosefu wa ajira tangu idadi kubwa ya viwanda kusitisha operesheni mjini Nakuru.

Kulingana na utafiti Kenya ilikuwa ikizalisha asilimia 80 ya pareto kote duniani, lakini kufikia sasa ni asilimia moja tu inayofika kwenye soko la kimataifa.

You can share this post!

HYRAX HILL: Makavazi ya kipekee Nakuru

BI TAIFA MEI MOSI, 2019

adminleo