Shughuli mahakamani zasitishwa kupisha uchaguzi wa mawakili
Na RICHARD MUNGUTI
SHUGHULI katika mahakama za Nairobi zilisimamishwa Alhamisi na uchaguzi wa mawakili uliofanyika kote nchini.
Katika mahakama ya Milimani Nairobi kesi nyingi ziliahirishwa kwa vile mawakili walikongamana katika maegesho ya Mahakama ya Juu na Mahakama Kuu kuwachagua viongozi wao.
Nyadhifa zilizowaniWa ni kadhaa lakini ule wa urais wa chama cha mawakili nchini LSK ulizua utata mkali kwa vile wakili Nelson Havi aliwasilisha kesi akiomba jina lake lichapishwe katika makaratasi ya kura.
Vibanda vya kupigia kura viliwekwa katika maegesho ya Mahakama ya Juu na Mahakama Kuu.
Milolongo mirefu ya mawakili ilishuhudiwa katika mahakama hizi mbili.
“Leo ni kama tuko na sikukuu. Hatuendi kortini kuwatetea wateja wetu. Tunatekeleza majukumu yetu kuwachagua viongozi,” Wakili Bernard Koyyoko aliambia Taifa Leo katika Mahakama ya Milimani.
Kesi nyingi katika korti za mahakimu na majaji ziliahirishwa kuwezesha mawakili kushiriki katika zoezi lao.
Wadhifa wa urais unawaniwa na mawakilI Aggrey Mwamu na Allan Gichuhi.
Mawakili 9,009
Mawakili wapatao 9,009 walishiriki katika zoezi hilo la kuwachagua wawakilishi wao katika kamati mbalimbali ikiwa ni pamoja na ile ya kusikiza mawakili wasio na nidhamu.
Mabw Mwamu na Gichuhi wanang’ang’ania kuona atakayemrithi rais wa sasa Isaac Okero.
Katika kesi ambayo Bw Havi aliwasilisha alikuwa akiomba mahakama ishurutishe LSK kuweka jina lake katika makaratasi ya kura. LSK ilipinga kesi hiyo ikisema hajahitimu.
Jaji John Mativo alisikiza kesi hiyo na kuitupilia mbali akisema hajatimiza miaka 15 inayotakiwa kwa mmoja kufaulu kuwania urais wa LSK.
Akitupilia mbali kesi ya Bw Havi, Jaji Mativo alisema LSK hakikukosea kilipokataa kuchapisha jina la Bw Havi kwenye makaratasi ya kura.