Kisumu All Stars waweka hai tumaini la kutinga KPL baada ya kulaza Police

Na GEOFFREY ANENE

KISUMU All Stars ilijiongezea matumaini ya kuingia Ligi Kuu msimu 2019-2020 baada ya kubwaga Kenya Police 1-0 kwenye mechi yake ya 35 ya Ligi ya Supa uwanjani Moi mjini Kisumu, mnamo Jumatatu.

Wenyeji Kisumu, ambao walipoteza penalti moja, walipata bao la ushindi katika kipindi cha pili kupitia kwa Gerrishom Arabe na kupunguza mwanya kati yake na viongozi Wazito hadi alama nne.

Wazito, ambayo ilitemwa kutoka Ligi Kuu mwisho wa msimu 2018, inaongoza kwa alama 75 baada ya kusakata mechi 35 kwenye ligi hii ya timu 20.

Kisumu inasalia katika nafasi ya pili, ambayo ni ya mwisho ya timu kutoka Ligi ya Daraja ya Pili kufuzu moja kwa moja kushiriki Ligi Kuu.

Police, ambayo kichapo dhidi ya Kisumu kinatia doa katika kampeni yao ya kuingia Ligi Kuu, inasalia katika nafasi ya tano kwa alama 63.

Hata hivyo, Police bado iko katika vita vya kumaliza katika nafasi ya tatu ambavyo kwa wakati huu pia vinahusisha Kisumu, Nairobi Stima na Ushuru, huku Bidco United na FC Talanta zikiwa na nafasi finyu.

Timu itakayomaliza Ligi ya Supa katika nafasi ya tatu italimana na nambari 16 kutoka Ligi Kuu kuingia Ligi Kuu msimu ujao.

Habari zinazohusiana na hii