Hatimaye Bamburi yailipa KRA ushuru wa Sh332 milioni
Na BERNARDINE MUTANU
Kampuni ya saruji ya Bamburi imeilipa Mamlaka ya Kukusanya Ushuru (KRA) mamilioni baada kuzozana kwa miaka mingi kuhusu ushuru.
Kampuni hiyo ililipa KRA Sh332 milioni, kiwango cha chini ikilinganishwa na ushuru uliodaiwa na mamlaka hiyo 2012 wa Sh3.9 bilioni.
Hata hivyo, Bamburi bado inadaiwa ushuru wa Sh288 milioni, faini iliyotozwa na KRA. Kampuni hiyo hata hivyo imeomba kusamehewa.
Hatua hiyo iliafikiwa mwaka jana kulingana na ripoti ya kila mwaka ya kampuni hiyo.
“Mwaka huu tuliafikiana na KRA kuhusiana na ushuru wa miaka ya awali uliokumbwa na mizozo,” kampuni hiyo ilisema katika ripoti.
Kulingana na Bamburi, ushuru huo ulilipwa 2018. Hatua hiyo ilichukuliwa miezi kadhaa baada ya aliyekuwa afisa mkuu wa KRA Alice Owuor kujiunga na bodi ya Bamburi 2017.
Bi Owuor alijiunga na KRA 1984 na alihudumu katika viwango tofauti kabla ya kustaafu kama kamishna wa ushuru (wa nyumbani) 2016.
Awali, Bamburi ilikuwa imeomba KRA kuilipa Sh471 milioni baada ya kutakuwa kulipa ushuru wa jumla ya Sh3.9 bilioni (Sh2 bilioni na faini ya Sh1.9 bilioni) mwaka wa 2012.
Ushuru huo ulisemekana kuwa wa kati ya 2007 na 2011.