• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 2:07 PM
Wiper yaanza mbinu za kumwadhibu Kibwana

Wiper yaanza mbinu za kumwadhibu Kibwana

Na PIUS MAUNDU

KIONGOZI wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka, amevunja ushirikiano wa chama chake na kile cha Muungano katika hatua ya hivi punde ya kuendelea kudorora kwa uhusiano baina yake na Gavana wa Makueni Kivutha Kibwana.

Profesa Kibwana alihama chama cha Muungano alichokuwa akiongoza kabla ya uchaguzi mkuu wa 2017 baada ya kukubaliana na Bw Musyoka kumuunga mkono aweze kuimarisha nafasi yake katika muungano wa upinzani, NASA.

Vyama hivyo vilikuwa vikishirikiana licha ya manung’uniko na viliteua viongozi katika bunge la kaunti pamoja vikiwa na idadi kubwa ya madiwani.

Bw Musyoka amelaumu madiwani wa kaunti ya Makueni kwa kuwa waaminifu kwa Profesa Kibwana na anatarajia kwamba kuvunja ushirikiano wa vyama hivyo kutaimarisha ubabe wake kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022.

“Mkataba wa muungano ulikuwa wa mwaka mmoja na umepita. Tutaandikia msajili wa vyama vya kisiasa kumfahamisha kwamba hakuna uhusiano kati ya Wiper na Muungano. Hii itakomesha suala la uaminifu katika bunge la kaunti,” Bw Musyoka alisema mnamo Jumatatu akiwa eneo la Ikoyo, Kaunti ya Makueni ambapo alikutana na baadhi ya viongozi wa eneo hilo.

Hata hivyo, kiongozi wa chama cha Muungano, Bw Titus Muunda alikaribisha hatua ya Bw Musyoka akisema uhusiano wa chama chake na Wiper haukuwa mzuri.

“Muungano kilikubali kushirikiana na Wiper ili kuepuka upinzani kaunti ya Makueni kabla ya uchaguzi wa 2017.

Hata hivyo, hii haikuwezekana kwa sababu Wiper kimekuwa kikidharau vyama vidogo. Sisi wenyewe tulitaka kuvunja ushirikiano huo mapema. Kwa kutengana tutakuwa huru kushirikiana na yeyote katika siasa nchini,” Bw Muunda aliambia Taifa Leo kwenye mahojiano.

Chama cha Muungano kina madiwani 10 katika bunge lililo na madiwani 48 wengi wakiwa wa chama cha Wiper.

Kutengana kwa Wiper na Muungano kunatarajiwa kubadilisha uongozi katika bunge la kaunti kwa kupokonya vyama vidogo nyadhifa za viongozi wa wachache ambazo zitachukuliwa na madiwani wa Muungano.

Profesa Kibwana, ambaye alichaguliwa kwa tiketi ya chama cha Wiper ambacho aliongoza kwa muda akiwa mwenyekiti, alitofautiana na Bw Musyoka akimlaumu kwa kukosa kujitolea kuleta maendeleo katika eneo hilo. Bw Musyoka kwa upande wake analaumu gavana huyo kwa kukosa uaminifu kwake na kwa chama.

Kulingana na wadadisi wa siasa wanaofahamu maelezo ya mkataba wa Wiper na Muungano, Profesa Kibwana hawezi kufukuzwa Wiper vyama hivyo vikivunja ushirikiano wao.

Wakati huohuo Bw Musyoka amekumbatia baadhi ya waliokuwa madiwani wa kaunti ya Makueni waliokosana na Profesa Kibwana.

Miongoni mwao ni aliyekuwa spika wa bunge la kaunti ya Makueni Stephen Ngelu, aliyekuwa kiongozi wa wengi Francis Mutuku, aliyekuwa kiranja Jackson Ngovi na aliyekuwa naibu spika Bernard Musau.

You can share this post!

Kenya imeoza, yataka mageuzi ya dharura – Mudavadi

Hakimu ahofia washukiwa wa mauaji watauawa na polisi

adminleo