Habari MsetoSiasa

Lonyangapuo atetea naibu wake kuhudumia wakazi akiwa Amerika

May 29th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na PETER MBURU

GAVANA wa West Pokot Prof John Lonyangapuo amemtetea naibu wake Dkt Nicholas Atudonyang’ kutokana na hali yake kukosekana katika kaunti kwa muda mrefu, akisema hata akiwa nje ya nchi anaisaidia kaunti.

Dkt Atudonyang’ amekuwa nchini Marekani zaidi ya mwaka, hali ambayo imeibua malalamishi kutoka kwa baadhi ya wakazi wa kaunti hiyo, wakishindwa jinsi anafanya kazi akiwa US.

Hata hivyo, alipofika mbele ya Kamati ya Bunge la Seneti kuhudu Uhasibu Jumatano, Gavana Lonyangapuo alimtetea naibu wake vikali wakati alipotakiwa kueleza kuhusu hali hiyo na jinsi anaendesha kaunti.

“Naibu gavana hajakuwa nchini kwa miaka miwili tangu uchaguzi ulipokamilika. Anafanya kazi ya udaktari US,” seneta wa Mombasa Mohamed Faki akasema.

Prof John Lonyangapuo alipofika mbele ya Kamati ya Bunge la Seneti kuhudu Uhasibu Jumatano. Picha/ Peter Mburu

Lakini Prof Lonyangapuo alisema naibu wake alikuwa kama balozi wa kaunti yake nje ya nchi, akisema amekuwa akiisaidia kupata misaada ya vifaa vya matibabu.

Gavana huyo aidha alisema kuwa Dkt Atudonyang’ amekuwa akisafiri kutoka US na kufika katika kaunti mara kwa mara, kuona jinsi kazi inaendelea.

“Yeye ni balozi mzuri wa kaunti kwa kuwa anatuletea vifaa vya matibabu vya msaada. Vilevile, hatuna changamoto yoyote katika kaunti,” akasema Prof Lonyangapuo.

Aidha, gavana huyo alisema kuwa naibu wake halipwi mshahara na hivyo hakuna mtu anayefaa kumkosoa kwa kutokuwa katika kaunti, akisema msaada wake umekuwa mkubwa anapokuwa nje ya nchi.

Aliwataka maseneta kuunda sheria inayowapa manaibu gavana kazi mahususi, ikiwa wanahisi kuwa baadhi ya kaunti haziendeshwi jinsi inavyofaa.

“Naibu wangu ndiye naibu gavana pekee nchini ambaye halipwi mshahara,” akasema.