• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Kampuni yachukua jukumu la kumtibu kibarua aliyeumwa na mbwa

Kampuni yachukua jukumu la kumtibu kibarua aliyeumwa na mbwa

Na LAWRENCE ONGARO

KUFUATIA habari zilizoangaziwa kwenye vyombo vya habari kuhusu mwanamume kushambuliwa na mbwa ‘sehemu nyeti’, kampuni ya Kahawa ya Kofinaf Coffee, imechukua jukumu la kumtibu.

Bw Justus Mwangi (pichani akiwa na mamake), ambaye ni kibarua kwenye kampuni hiyo alishambuliwa na mbwa na kujeruhiwa vibaya sehemu zake za siri.

Waandishi wa habari walipozuru kwao nyumbani katika kijiji cha Murera, Ruiru, Bw Mwangi alithibitisha kuwa kampuni hiyo ilichukua jukumu la kumpeleka hospitali ya kibinafsi mjini Thika kwa matibabu zaidi.

“Nimefurahi kwa sababu kampuni ya Kofinaf Coffee imechukua jukumu la kunipeleka hospitali kupata matibabu zaidi,” alisema Jumatano na kuongeza, “Wamesema watafanya ushirikiano ili nipate nafuu haraka.”

Meneja mkuu wa wa kampuni hiyo Bw Michael Gitau, alisema mnamo Jumanne, walimpeleka kibarua huyo kwa matibabu ya dharura ambapo alifanyiwa uchunguzi wa X-Ray huku ikithibitishwa kuwa alipata majeraha mabaya.

“Tutahakikisha Bw Mwangi anatibiwa hadi apone kabisa ambapo kampuni itagharimia mahitaji yote ya hospitali. Baadaye tutafanya juhudi arudi kufanya kazi kwetu,” alisema Bw Gitau.

Aliomba radhi kwa kile kilichotendeka huku akisema tayari wameanza kuendesha uchunguzi wao wenyewe kuthibitisha hasa ni nini kilijiri hadi kibarua huyo akaumwa na mbwa wa kampuni hiyo.

Afisa mkuu wa usalama Bw Thomas Wekesa (kulia) na shati jeupe akimpeleka Bw Justus Mwangi hospitalini baada ya kushambuliwa na mbwa. Picha/ Lawrence Ongaro

“Tutahakikisha askari aliyefanya kitendo hicho cha unyama anachukuliwa hatua ya kisheria. Hatuwezi kukubali askarirungu wafanye kazi yao kiholela bila kujali wafanyakazi wetu,” alisema Bw Gitau.

Alisema askari wapatao watano wa kampuni hiyo tayari wameandikisha taarifa huku uchunguzi ukiendelea.

Alisema wizi wa kahawa umekuwa Mwingi ambapo wezi hutumia pikipiki kuiba na kutoroka mara mmoja.

“Hiyo ndiyo maana mara nyingi hatuwaruhusu wahudumu wa bodaboda kuingiza pikipiki ndani ya kiwanda chetu,” alisema Bw Gitau.

Afisa mkuu wa usalama Bw Thomas Wekesa, alisema kwa miezi michache iliyopita shamba lao kubwa la Kofinaf Coffee, na mengine yaliyoko karibu yanatumiwa kama dampo la maiti baada ya wahanga kuuawa kwingineko.

“Kwa muda wa wiki mbili zilizopita tumeokota miili ya watu zaidi ya watano. Miili hiyo huwa imefungwa mikono kwa nyuma huku vichwa vikiwa vimefungwa ndani ya karatasi ya nailoni,” alisema Bw Wekesa.

Hili ndilo shamba la Kahawa la Kofinaf mjini Ruiru. Picha/ Lawrence Ongaro

Alisema tayari wamewasiliana na maafisa wa usalama ili kuchunguza visa vya aina hiyo.

“Hata tayari uchunguzi umeanzishwa kwa sababu inashukiwa pengine watu hao huuliwa sehemu za mbali kama Murang’a, Nairobi na kwingineko halafu baadaye wanasafirishwa hadi kwa mashamba yetu hapa,” alisema Bw Wekesa.

Alisema pia wameweka ulinzi mkali kwenye mashamba hayo kwa minajili ya kuzuia wezi wa kahawa ambao huja usiku ili kuiba kahawa hiyo ambayo ina gredi ya juu katika soko.

You can share this post!

IEBC yasubiriwa kuidhinisha sahihi za Thirdway Alliance...

Danny Rose haamini Spurs wamo fainalini

adminleo