Habari

Mvua kubwa yasababisha maafa kote nchini

March 5th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na WAANDISHI WETU

Kwa ufupi:

  • Watu watatu waliaga dunia na wengine zaidi ya 150 wakaachwa bila makao Taita Taveta
  • Katika Kaunti ya Tharaka Nithi, mama na wanawe wawili walifariki walipopigwa na radi wakiwa nyumbani kwao
  • Barabara kadhaa katika kaunti za Turkana, Pokot Magharibi, Baringo na Elgeyo Marakwet hazipitiki kabisa
  • Mamia ya wasafiri walilala njiani usiku wa kuamkia jana kutokana na msongamano wa magari uliodumu kwa zaidi ya saa 20 kwenye barabara ya Mombasa – Nairobi

MVUA iliyotarajiwa kuwa baraka kwa Wakenya imesababisha maafa makubwa huku watu saba wakifa kutokana na mafuriko, nyumba na mimea ikisombwa nao usafiri ukitatizika.

Katika Kaunti ya Taita Taveta, watu watatu waliaga dunia na wengine zaidi ya 150 wakaachwa bila makao. Kati ya waliokufa ni mzee wa miaka 96, Badi Hussein, ambaye nyumba yake ilisombwa na mafuriko kijijini Wanganga eneo la Mata, Taveta.

Naibu wa chifu wa Timbila, Bw Corneil Salehe, alisema mkongwe huyo alikuwa akiishi peke yake.

Mmoja wa wakazi, Nashon Nasula alisema mvua kubwa pia iliharibu nyumba, mifugo na mimea na kulazimu wengi kulala nje kwenye baridi.

OCPD wa Taveta, Simon Gababa alisema awali raia wa Tanzania alikufa nyumba yake ilipoanguka akiwa amelala kutokana na mvua kubwa kijijini Msengoni.

 

Mauti ya radi

Katika eneo la Sofia kaunti ndogo ya Voi, mwanamke wa miaka 66 alipigwa na radi nje ya nyumba yake. OCPD wa eneo hilo, Fred Ochieng aliwaomba wakazi kuhama maeneo yenye mafuriko.

Katika Kaunti ya Tharaka Nithi, mama na wanawe wawili walifariki walipopigwa na radi wakiwa nyumbani kwao.

Katika kaunti ya Kisumu mtu mmoja alifariki baada ya kusombwa na maji ya mvua Jumamosi usiku. Mwili wa marehemu ulipatikana kwenye kingo za chemichemi eneo la Manyatta.

Chifu wa eneo hilo, Bw Charles Odondo alisema marehemu ambaye huenda alikuwa mlevi wakati wa mkasa, hajatambuliwa jina.

Maafisa wa polisi wakipeleka mochari mwili wa mwanamume aliyefariki baada ya kusombwa na maji katika mtaa wa Manyatta, Kisumu Machi 4, 2018. Picha/ Ondari Ogega

Kaskazini mwa Bonde la Ufa, usambazaji chakula cha misaada umeathiriwa sana na mafuriko makubwa ambayo yameharibu barabara nyingi.

Hilo limezua hofu ya maelfu ya familia nyingi kuendelea kukabiliwa na ukosefu wa vyakula kwani hazifikiwi.

Barabara kadhaa katika kaunti za Turkana, Pokot Magharibi, Baringo na Elgeyo Marakwet hazipitiki kabisa, hali ambayo imeathiri sana utoaji wa misaada ya kibinadamu.

“Matrela yanayobeba vyakula na misaada hayafikii maeneo hayo kutokana na hali mbaya za barabara. Hilo linaziweka familia hizo katika hatari ya kuendelea kukabiliwa na njaa,” akasema Naibu Kamishna wa Kaunti Ndogo ya Kibish, Eric Wanyonyi.

 

Misongamano

Kwenye barabara ya Mombasa – Nairobi, mamia ya wasafiri walilala njiani usiku wa kuamkia jana kutokana na msongamano wa magari uliodumu kwa zaidi ya saa 20. Msongamano huo ulitokana na mvua kubwa iliyotatiza madereva.

Msongamano huo ulioanza saa nne za usiku wa Jumamosi ulikuwa haujatatuliwa kufikia saa saba za mchana jana.

Matrela, mabasi na matatu pamoja na magari ya kibinafsi yalijazana barabarani kutoka Athi River hadi makutano ya Chumvi.

Kamanda wa trafiki wa Machakos, Abdinasir Harun, alisema walikuwa wanafanya kila juhudi kumaliza msongamano huo.

Msongamano huo ulitatiza wanafunzi waliokuwa wakirejea shuleni maeneo ya Machakos na Makueni kutokana na uhaba wa magari. Katika kituo cha mabasi cha Railways, wanafunzi waliokuwa wakielekea Machakos walilazimika kulipa nauli ya Sh500 badala ya Sh200 zinazotozwa siku za kawaida.

Misongamano zaidi ilishuhudiwa kwenye barabara nyingi za Nairobi kama vile Kiambu, Ruiru na Eastern Bypass, ambapo wengi walilalamika kukaa hadi saa tatu wakiwa wamekwama.

Mafuriko pia yaliripotiwa katika eneo la Suswa kwenye barabara ya Narok-Mai Mahiu hapo Jumapili na kutatiza usafiri.

Ripoti za BARNABAS BII, WINNIE ATIENO, VICTOR OTIENO, STEPHEN MUTHINI, ALEX NJERU na LUCY MKANYIKA