Kiunjuri aonya Mlima Kenya kwa kugawanyika
Bw Kiunjuri aliwaonya viongozi dhidi ya kufuata baadhi ya makundi ya kisiasa bila tahadhari.
Alisema kuwa migawanyiko miongoni kwa viongozi inahatarisha nafasi ya eneo hilo kuwa katika serikali zijazo.
Akizungumza kwa mafumbo kwa lugha ya Gikuyu alipohutubu katika Kaunti ya Murang’a Alhamisi, Bw Kiunjuri alisema kuwa amehudumu katika serikali za marais wastaafu Daniel Moi, Mwai Kibaki na sasa Uhuru Kenyatta, ambapo kuna hatari kwa jamii hiyo kukosa kuwakilishwa katika serikali zijazo ikiwa wataendelea kugawanyika kisiasa.
“Nina tajriba ya kutosha kuhusu siasa za Kenya na tamaduni ya jamii ya Agikuyu, ambayo haituruhusu kuonyesha tofauti zetu hadharani,” akasema huku wakazi wakifuatilia kwa makini.
“Viongozi lazima waelewe kwamba kulingana na utamaduni ya jamii ya Agikuyu, mbuzi hapeanwi na ngozi yake, kumaanisha kuwa lazima mtu ajiwekee akiba. Ikiwa hatutaungana na kujadiliana kuhusu mwelekeo wa kisiasa tutakaochukua, huenda tukaanza kujuta kwa kutengwa kama ilivyokuwa wakati wa enzi ya Rais Mstaafu Moi,” akasema.
Na ijapokuwa hakutaja yeyote, matamshi yake yalionekana kuyalenga makundi ya kisiasa ya ‘Kieleweke’ na ‘Tangatanga.’
Kundi la ‘Kieleweke’ linapinga nia ya Naibu Rais William Ruto kuwania urais mnamo 2022, huku lile la ‘Tanga Tanga’ likiendeleza kampeni zake kali kwa kumuunga Ruto na kumpinga aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga.