SRC yapinga kortini marupurupu ya wabunge
Na WALTER MENYA
HUENDA wabunge wakalazimika kurejesha mamilioni ya pesa ambazo walikuwa wamepokea kama marupurupu ya nyumba ikiwa Tume ya Kukadiria Mishahara (SRC) itashinda katika kesi ambayo imewasilisha kortini.
Ijumaa, tume hiyo kupitia wakili Peter Wanyama ilifika katika Mahakama Kuu kuwasilisha ombi ikitaka hatua ya kuwalipa marupurupu hayo ibatilishwe, na pesa ambazo tayari wamelipwa zirejeshwe.
SRC inataka korti kuwaamrisha makarani wa Bunge la Taifa na la Seneti “kurejesha pesa zote ambazo zimelipwa kama mishahara na marupurupu kwa wabunge na maseneta, kupitia uamuzi ambao inautaja kuwa kinyume cha katiba na maelekezo ya tume.”
Aidha, SRC inaitaka korti kuwafanya wanachama wa Tume ya Huduma za Bunge (PSC) kuwajibika binafsi, pamoja na katibu wa tume hiyo Jeremiah Nyegenye, kwa kulipa marupurupu hayo bila kufuata sheria.
Wanachama wote wa PSC wameorodheshwa kama washtakiwa katika kesi hiyo; wakiwa spika Justin Muturi, Dkt Naomi Shaban, Seneta Maalum Beth Mugo, Adan Keynan, Benson Momanyi, George Khaniri, Aisha Jumwa, Aaron Cheruiyot, Dkt Lorna Mumelo na Bw Nyegenye.
Katika kesi hiyo, SRC inawalaumu wabunge kwa kukiuka katiba ambayo inaipa tume hiyo pekee jukumu la kuamua mishahara na marupurupu watakayolipwa maafisa wote wa umma.
“Uamuzi wa PSC kutenga na kuwalipa wabunge na maseneta marupurupu ya nyumba ni kukiuka sheria, vilevile ni kukiuka katiba kuwa SRC ndiyo pekee inayofaa kuamua malipo kwa maafisa wote wa umma,” SRC inasema katika kesi hiyo.
“Maafisa ambao wamefadhiliwa kununua nyumba na serikali, hawafai kulipwa marupurupu ya nyumba,” SRC inasema.
Marupurupu
Wabunge na maseneta hivi majuzi walijiongezea Sh250,000 kila mmoja, kwa mwezi kama marupurupu ya nyumba na kupitisha kuwa pesa hizo zianze kulipwa kuanzia Oktoba 2018.
Lakini SRC inadai kuwa hatua hiyo itagharimu nchi Sh99.5 milioni kila mwezi na Sh1.194 bilioni kila mwaka.
“Uamuzi wa PSC unatoa mwongozo mbaya kuhusu jinsi pesa za umma zinavyofaa kusimamiwa,” tume hiyo inasema.
Aidha, SRC inasema kwa sasa wabunge wanalipwa vyema, mishahara ya kawaida na marupurupu mengine yakiunganishwa.
Kwa mfano, kila wiki wabunge hulipwa Sh109 kwa kila kilomita wanayosafiri kwenda maeneobunge yao, pamoja na marupurupu ya kila mwezi ya kutunza gari ya Sh356,525.
“Aidha, wanapata marupurupu mazuri ya afya yao wenyewe, wake wao ama waume wao na watoto hadi wanne wenye chini ya miaka 25. Vilevile wanapata marupurupu ya pesa za simu, bima za ajali na kuhudhuria vikao vya bunge na kamati za bunge.” Wanachama wa kawaida katika kamati hulipwa marupurupu ya Sh5,000 kwa kila kikao cha kamati ambacho wanahudhuria, na Sh8,000 kwa mwenyekiti wa kamati.
Aidha, wana bima ya matibabu ya Sh10 milioni ya kulazwa) na Sh300,000 (ya kutibiwa na kuruhusiwa kwenda nyumbani), mkopo wa Sh7 milioni kununua gari, wa hadi Sh20 milioni kununua nyumba, Sh15,000 za kutumia simu, pamoja na usalama.