Makala

TAHARIRI: Dosari katika vitabu zirekebishwe haraka

March 6th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

WANAFUNZI wa Kidato cha Kwanza katika shule ya Moi Girls, Eldoret wakionyesha vitabu walivyopewa chini ya mpango wa Serikali mapema mwaka huu. Walimu wamelalamika kuwa baadhi ya vitabu hivyo vina makosa yanayopotosha wanafunzi.
Picha/Jared Nyataya

Na MHARIRI

KUIBUKA kwa habari kwamba kuna kasoro nyingi kwenye vitabu vinavyotumiwa na wanafunzi ni jambo la kvunja moyo.

Walimu wanasema walianza kugundua makosa mengi mara walipopewa vitabu hivyo, na sasa wamelazimika kuviweka kando na badala yake wanatumia vingine ili wasipotoshe wanafunzi wao.

Vitabu hivyo vilivyogharimu Sh7.5 bilioni vilipeanwa kwa wanafunzi wa Kidato cha Kwanza chini ya mpango wa Elimu Bila Malipo. Usambazaji wa vitabu hivyo ulizinduliwa rasmi na Rais Uhuru Kenyatta katika Ikulu ya Nairobi mnamo Januari 5 mwaka huu na kufikia sasa vimesambazwa kwa wanafunzi wa shule za umma.

Malalamishi mengi zaidi yametoka kwa walimu wa Kiswahili, ambao wanasema mojawapo ya vitabu walivyopewa, kilichapishwa kwa haraka na kampuni moja mashuhuri ya uchapishaji nchini.

Makosa yaliyopatikana katika baadhi ya vitabu vya Kiswahili ni kama vile mifano potovu ya vivumishi, nomino, vitenzi na utumizi wa vipengele ambavyo havitambuliki katika lugha. Pia walimu wanasema mpangilio wa mada unakanganya.

Kulingana na walimu, kazoro hizo pia zimo kwenye vitabu vya masomo ya Kiingereza, Hesabu, Fizikia, Kemia na Biolojia.

Matatizo mengine yaliyopo yanahusu ufinyu wa mada. Hakuna maelezo ya kina. Wachapishaji waliharakisha bila kupitia ile kazi waliyokuwa wakichapisha.

Hii inaathiri wanafunzi kwa sababu wanasoma mambo ambayo hayawafai ama yanawapotosha

Afisa anayesimamia utafiti katika Taasisi ya Kenya ya Uundaji wa Mtaala (KICD), Bw Cyril Oyuga, amekiri kwamba taasisi hiyo imefahamu kuna dosari katika baadhi ya vitabu na tayari kuna mikakati iliyowekwa kusahihisha makosa.

Maadamu maafisa wa KICD wamekiri kuwepo kwa kasoro hizo, ipo haja kwa wao kuamuru vitabu hivyo vikusanywekuharibiwa, ili viandikwe tena kwa utaratibu.

Inaeleweka kuwa huenda kampuni za uchapishaji ziliharakishwa na zikawaharakisha waandishi, lakini maadamu kosa limeshajulikana, kilicho muhimu sasa ni kutolirudia.

Elimu ni jambo muhimu na msingi wa maisha kwa kila binadamu. Kile anachofunzwa mwanafunzi shuleni, humpa mwelekeo wa kufuata anapomaliza masomo.

Itakuwa busara ikiwa wanaohusika na masuala ya vitabu watachukua muda kupitia kila neno ndani ya vitabu vitakavyorekebishwa, ili wanafunzi wasipotoshwe.