• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 9:50 AM
Acha kutajataja Raila, wabunge wamuonya Ruto

Acha kutajataja Raila, wabunge wamuonya Ruto

Na RUTH MBULA na JOSIAH ODANGA

VIONGOZI wa ODM kutoka Nyanza wamemtaka Naibu Rais William Ruto akome kumdharau kiongozi wa chama chao Raila Odinga.

Wabunge wa chama hicho walimtaka Dkt Ruto kukoma kutaja jina la Bw Odinga katika hafla zake.

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa chama hicho Junet Mohammed, Mkurugenzi wa Masuala ya Kisiasa Opiyo Wandayi, Mwakilishi wa Wanawake Kaunti ya Homa Bay, Gladys Wanga na Mbunge wa Alego Usoga Samuel Atandi walisema Naibu Rais amekuwa na tabia ya ‘kumtusi’ Bw Odinga kila akipata nafasi na wakamtaka akome.

Wakiongea katika eneobunge la Suna Mashariki, Kaunti ya Migori mnamo Ijumaa wakati wa harambee katika shule ya Upili ya Onyalo, viongozi hao walimtaka Bw Ruto kuheshimu viongozi wakongwe nchini.

Walisema mtindo wa maisha wa Dkt Ruto unafaa kuchunguzwa, alivyoagiza Rais Uhuru Kenyatta awali sawa na ya wanasiasa wote.

Wanasiasa hao walisema Dkt Ruto anajisawiri kuwa masikini ilhali ana mali nyingi.

Wakati wa kuadhimisha siku ya maombi ya kitaifa Nairobi, Alhamisi, Dkt Ruto alisema amekulia katika umasikini na kutia bidii hadi alipo sasa.

Hata hivyo, viongozi hao walisema Bw Ruto ni tajiri anayejificha katika ‘hadithi’ ya umasikini.

“Ikiwa alikuwa masikini, sio masikini tena. Ana mahoteli makubwa jijini na hakuna masikini yeyote anayeweza kuwa na biashara kama hizo. Ana mashamba makubwa na anamiliki ndege, yeye ni masikini kweli?” aliuliza Bw Mohammed.

Kifo

Wakati wa maombi ya kitaifa, Bw Ruto alisema awali alikuwa mchungaji wa mifugo lakini amebarikiwa na kuwa kiongozi wa hadhi anayeketi na watoto wa waliokuwa watu mashuhuri.

Alieleza jinsi alivyopokea habari za kifo cha Rais wa kwanza wa Kenya, Hayati Mzee Jomo Kenyatta akiwa kijana mdogo.

“Niliposikia taarifa hiyo, nilikuwa nikichunga ng’ombe. Nilikimbia nyumbani kwa kufikiria kuwa ulikuwa mwisho wa dunia,” alisema.

“Licha ya kuwa utotoni sikuwa nikivaa viatu, leo ninaweza kuketi katika meza kuu na mwana wa rais mwanzilishi wa taifa la Kenya,” alisema na kuongeza kuwa wananchi ndio waliompa motisha wa kupanda ngazi.

Bw Wandayi alisema, kama taifa, tunafaa kuelewa tunakotoka na tunakoelekea.

“Kwa sababu kiongozi wetu ametuonyesha njia, ni muhimu kumheshimu kwa sababu ana nia njema kwa Kenya,” alisema mbunge huyo wa Ugunja.

Alisema Bw Odinga hakuwa mwenda wazimu kuamka tu siku moja na kusalimiana na Rais Uhuru Kenyatta.

Dkt Ruto alisema amekuwa akipinga muafaka wa Rais Kenyatta na Bw Odinga na vita dhidi ya ufisadi.

Bi Wanga alisema Wakenya, wawe matajiri au masikini, wana sababu ya kuomba na kumshukuru Mungu.

Kulingana na Bi Wanga, Bw Ruto anafaa kueleza alikotoa mali, hasa kutokana na hadithi yake ya kila mara kuwa ametoka familia masikini.

You can share this post!

Waliosajiliwa Huduma Namba ni 37.7 milioni – Uhuru

Shujaa yaponea shoka kwenye Raga ya Dunia baada ya kuingia...

adminleo