Makala

NASAHA ZA RAMADHAN: Khutba ya Swala ya Idd hutolewa tu baada ya watu kuswali

June 1st, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na SHEIKH MOHAMED KHALIFA

TUNAPOELEKEA ukingoni mwa mwezi huu Mtukufu wa Ramadhani, kilicho fikirani mwa waumini kote ulimwenguni ni kilele cha sherehe za kuadhimisha tukio hilo.

Jana nilieleza kwamba kukamilika kwa Ramdhani ni mojawapo ya furaha mbili anazopata mfungaji.

Furaha hii huanza asubuhi ya siku ya Idd (ambayo yaweza kuwa kesho kutwa Jumanne au Jumatano).

Siku hiyo hutanguliwa na watu kuenda kuswali swala ya Idd. Ni sunnah kubwa kabisa ambayo Mtume Muhammad (S.A.W) aliisisitiza kiasi kwamba hata wanawake walio katika hali zao za kila mwezi, huhimizwa wajumuike na wenzao, wakae nyuma kuonyesha umoja wakati wa swala ya Idd.

Yapo mambo kadhaa ya kuzingatia wakati wa swala hii.

Kwanza ni bora zaidi kwa swala hii kufanywa kwenye uwanja, isipokuwa kama kutakuwa na hali mbaya ya hewa kama vile mvua au upepo mkali.

Watu wanahimizwa kutumia njia tofauti ya kwenda uwanjani na nyingine wakati wa kuondoka.

Hekima iliyopo ni kuwa kwanza malaika hujipanga kuwasalimia na kuwatakia mema waumini.

Pili, kwa kupita kutumia njia tofauti ya kuenda na kurudi, Waislamu huonekana na watu wengi zaidi na kuvumisha siku hiyo kuu yenye furaha.

Mtu baada ya kuwa alifunga mwezi mzima, yafaa ashiriki katika swala hii.

Katika mojawapo ya sunna ni kuvaa nguo mpya. Unaoga, unavaa nguo yako mpya na kula kitu kabla ya kuanza kuondoka na kuenda katika uwanja.

Ni swala ya rakaa mbili. Ukienda uwanjani si sawa na msikitini na kwa hivyo ukifika unaketi. Huswali rakaa mbili za Tahiyatul Masjid.

Kwenye kila rakaa ya swala hii, Imamu hupiga takbira kadhaa kabla ya kuanza kusoma Suratul Fatiha.

Kwa mfano katika rakaa ya kwanza anaweza kupiga takbira saba na katika rakaa ya pili takbira tano kwa kusema “Allahu Akbar” mara hizo.

Swala inapokamilika, Imamu hupanda kwenye mimbar na kuanza kutoa khutba, ambapo katika swala ya Ijumaa khutba ndiyo inayoanza.

Mada ya khutba yapaswa kuhusiana na masuala muhimu ya siku ya Idd kama vile kuwajali masikini, kuwalisha mayatima, kusherehekea sikukuu kwa kuchunga mipaka aliyoiweka Mwenyezi Mungu na kadhalika.