• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 8:55 AM
JAMVI: Ruto aanza kuzima vyama hasimu kabla ya 2022

JAMVI: Ruto aanza kuzima vyama hasimu kabla ya 2022

 Na BENSO MATHEKA

HATUA ya aliyekuwa naibu kiongozi wa chama cha Ford Kenya Boni Khalwale ya kuhamia Jubilee ni mbinu ya Naibu Rais William Ruto ya kutaka kuzima vyama vya mahasimu wake wake wa kisiasa kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022, wadadisi wanasema.

Wanasema kwamba mbinu hii inalenga kufifisha vyama hivyo kabla ya kampeni za uchaguzi mkuu wa 2022 kuanza rasmi japo kwa wakati huu anaendelea kujipigia debe kote nchini.

Hata hivyo, baadhi ya wachanganuzi wa siasa wanasema kwamba ikizingatiwa kwamba ni miaka mitatu kabla ya uchaguzi mkuu na kwamba siasa za Kenya ni telezi, kibarua kitakuwa ni kudumisha ukuruba wake wa kisiasa na wanasiasa anaoshawishi kujiunga na katika kambi yake.

“Tumeona akilenga vyama vikuu vya kisiasa eneo la Magharibi ambapo amenasa manaibu wa vyama vya Ford Kenya na Amani National Congress. Lengo la kufanya hivi ni kutaka kuviporomosha kabla ya uchaguzi mkuu ujao kwa kulenga viongozi na wanachama wenye ushawishi,” asema mdadisi wa kisiasa Geff Kamwanah.

Aliyekuwa naibu kiongozi wa chama cha Ford Kenya Boni Khalwale alijiunga na kambi ya Bw Ruto katika chama cha Jubilee maarufu kama Tanga Tanga baada ya kushirikiana na mrengo huo kwa muda.

Kuhama kwake kulijiri wakati ambao chama cha Ford Kenya kilikuwa kimetisha kumwadhibu kwa kushirikiana naTanga Tanga.

Naibu kiongozi wa chama cha ANC, Bw Kipruto Arap Kirwa ambaye kwa miaka mingi amekuwa hasimu kwa kisiasa wa Naibu Rais Ruto pia ametangaza kwamba atajiunga Tanga Tanga baada ya kuzika totauti zake na Dkt Ruto.

Kulingana na Bw Kamwanah, kwa kulenga manaibu wa vyama vikubwa vya kisiasa eneo la Magharibi Dkt Ruto anataka kupenya zaidi eneo hilo ambalo limekuwa likimpigia kura kwa wingi kiongozi wa upinzani Raila Odinga.

“Analenga watu ambao japo wanaweza kupuuzwa kwa kutokuwa serikalini, wana ushawishi au anataka kuwatumia kupiga vita mahasimu wake wa kisiasa.

Pili, anajua kwamba watu anaolenga wameshikilia vyama wanavyohama kwa njia moja au nyingine,” asema.

Anataja Bw Kirwa ambaye Bw Mudavadi alimteua naibu wa kiongozi wa chama cha ANC ili kuwa na mwakilishi katika eneo North Rift wakati ambao yeye ( Kirwa) na Dkt Ruto walikuwa wametofautiana vikali.

Bw Kirwa anatoka eneo la Cheragany linalowakilishwa na Joshua Kutuny mmoja wa wanachama wa kundi la Kieleweke linalompiga vita Dkt Ruto katika chama cha Jubilee.

Wadadisi wanasema kwamba kwa kuvutia viongozi wa vyama vya kisiasa upande wake, Dkt Ruto atakuwa katika hali nzuri ya kuelewa siri na mikakati ya vyama pinzani anapojiandaa kugombea urais 2022.

“Ninachojua ni kwamba ameelekeleza juhudi zake kuporomosha vyama vya kisiasa maarufu katika ngome za Bw Odinga nje ya Nyanza na kwa hivyo sio ajabu amenasa Bw Khalwale na Bw Kirwa,” aeleza mdadisi wa masuala ya kisiasa George Ambani.

Mdadisi huyu anasema Dkt Ruto anawatumia viongozi anaonasa kupiga vita vyama wanavyotoka.

“Kwa mfano, ulimsikia Bw Khalwale akisema Bw Mudavadi na Bw Wetangula ni viongozi wasio maarufu kitaifa na kukosoa muungano wa NASA. Matamshi kama haya ni mikakati ya Dkt Ruto ya kuangamiza miungano ya vyama vya kisiasa huku akilenga kuunda muungano mpya kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022,” alisema Bw Ambani.

Akizungumza katika kipindi cha Point Blank katika runinga ya KTN mnamo Jumanne usiku, Bw Khalwale alisema Tanga Tanga limejiandaa kuunda chama au muungano mpya iwapo chama cha Jubilee kitasambaratika kabla ya uchaguzi mkuu ujao.

“Matamshi haya yanaonyesha kuwa Dkt Ruto anavua wanasiasa wenye ushawishi katika vyama vya kisiasa ili atakapotangaza muungano wake asiwe na kibarua kuwatambulisha kwa wapigakura,” aeleza Bw Ambani.

Wadadisi wanasema kuwa Dkt Ruto ni mwanasiasa machachari, anayejua kupanga mikakati yake ya kisiasa vilivyo na asiyepesa kuchukua hatua inayomfaidi kisiasa.

“Kwamba yuko mamlakani kama Naibu Rais wa Kenya na kwamba ana uwezo wa kifedha na ni mnenaji shupavu, unaweza kutarajia wanasiasa zaidi hasa walio kwenye baridi ya kisiasa kutema vyama vyao na kujiunga naye kabla ya uchaguzi mkuu ujao,” asema Bw Kamwanah.

Bw Ruto amevutia wabunge kadhaa wa vyama vya upinzani eneo la Pwani upande wake na alikuwa kwenye msitari wa mbele kushawishi mgombeaji wa chama cha ODM kwenye uchaguzi mdogo wa kiti cha Wajir Magharibi Mohammed Elmi kujiondoa na kujiunga na Jubilee.

Kuna minong’ono kwamba huenda kuna mkono wake katika tofauti kati ya kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka na aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho Profesa Kivutha Kibwana. Profesa Kibwana alimtembelea Dkt Ruto katika ofisi yake mwaka jana kabla ya kuzuka kwa tofauti kati yake na Bw Musyoka.

You can share this post!

JAMVI: Rais Kenyatta anavyopotoshwa na washauri wake

JAMVI: ‘Kieleweke’ kutaka kutambuliwa Bungeni...

adminleo