• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 6:55 PM
Kaunti yafadhili familia 16,870 kwa NHIF

Kaunti yafadhili familia 16,870 kwa NHIF

NA KALUME KAZUNGU

FAMILIA 16,870 ambazo hazijiwezi zimepokea kadi za Bima ya Afya ya Hospitalini (NHIF) chini ya udhamini mkuu wa serikali ya kaunti ya Lamu.

Shughuli ya kugawanya kadi hizo kwa familia zilizosajiliwa kwa mpango huo kwenye sehemu mbalimbali za Lamu ilizinduliwa rasmi na Naibu Gavana wa Lamu, Abdulhakim Aboud eneo la Mkunguni kisiwani Lamu.

Awali, serikali ya kaunti ya Lamu ilikuwa imeahidi kufadhili familia 20,000 zisizojiweza ili kufaidi mpango huo wa NHIF hukui jumla ya Sh 120 milioni zikitengwa ilio kufanikisha programu hiyo.

Akizungumza wakati wa kukabidhi kadi kwa familia zilizonufaika, Bw Aboud alisema shughuli ya usajili wa zaidi ya familia 3000 zilizosalia bado inaendelea kote Lamu na akawataka wakazi kujitokeza kusajiliwa ili kunufaika na bima hiyo ya afya.

Bw Aboud alisema mpango huo utahakikisha kila mkazi wa Lamu anafikia matibabu bora bila pingamizi zozote, ikiwemo zile za kifedha.

Mpango huo unalenga kuafikia ajenda nne kuu za serikali ya kitaifa, chini ya uongozi wa Rais Uhuru Kenyatta, mojawapo ikiwa ni wakazi wa tabaka zote kufikia huduma bora za afya hapa nchini (UHC).

“Tunafuraha kuanzisha zoezi la kuwapa wakazi waliojisajili kadi zao za NHIF. Kati ya familia 20,000 tunazolenga zinufaike na mpango huu, leo tuko na kadi 16,870 ambazo zitapewa familia husika ili kuanza kuzitumia.

|”Familia takriban 3,130 zilizobakia pia zitasajiliwa na kadi zao kutayarishwa na kukabidhiwa kwao rasmi hivi kariobuni. Cha msingi ni wakazi kujitokeza na kujiandikisha kwa mpango huu. Kadi zote zinafadhiliwa na kaunti kwa hivyo mkazi hatoi chochote,” akasema Bw Aboud.

Naye afisa Mshirikishi wa mpango wa Huduma ya Afya kufikia watu wote (UHC), kaunti ya Lamu, Abdulaziz Mwendwa alisema kadi hizo zitahudumia magonjwa yote kwa wale walio nazo kwani wanachohitaji tu ni kutoa kadi hizo ili kuhudumiwa kwenye hospitali zote za Lamu na hata nje.

Miongoni mwa walionufaika na mpango huo pia ni waathiriwa wa dawa za kulevya ambao sasa wataweza kutembelea vituo vya afya wakiwa na kadi zao ili kupewa ushauri na hata kutibiwa na kusaidiwa kujinasua kutoka kwa janga hilo la mihadarati.

“Nashukuru sana kaunti kwa kuibuka na mpango huu. Inamaanisha wananchi wote ambao awali hawajakuwa na uwezo wa kujisimamia kiafya sasa watasaidika,” akasema Bw Mwendwa.

You can share this post!

Nini hasa ndicho kiini cha mtu kujitia kitanzi?

Ruto arejea Kiambu akisema katumwa na Rais

adminleo