Habari Mseto

Hata mruke angani, marufuku ya makaa itadumu, aapa Gavana Ngilu

March 6th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Gavana Charity Ngilu akihutubia wanahabari nje ya mahakama kuu ya Milimani Machi 5, 2018. Picha/ Richard Munguti

Na RICHARD MUNGUTI

GAVANA wa Kitui Bi Charity Ngilu, Ijumaa alisisitiza kwamba hakuna kurudi nyuma katika kutekeleza amri ya kutochoma makaa.

“Hata wapande juu ya miti , ama waende baharini ama waruke angani, hata kufanyike nini, amri ya marufuku ya kukata miti na kuchoma makaa katika kaunti ya Kitui itadumu,” Bi Ngilu alisema punde tu mahakama ilipotupilia mbali kesi ya kupinga uchaguzi wake.

Wafuasi waliofuruka katika mahakama ya Milimani walimhakikishia Gavana huyo kwamba “watapambana na wachomaji makaa kwa kila hali.”

Bi Ngilu alisema marufuku hiyo ya makaa na usombaji changarawe itadumu.

“Kaunti ya Kitui imegeuzwa kuwa jangwa. Miti ya asili yote imekatwa na kuchomwa makaa na wafanyabiashara kutoka kaunti nyingine. Marufuku hii itadumu,” alisema Bi Ngilu huku akishangiliwa.

Bi Ngilu aliwashauri wakazi wote wa Kitui na jimbo lote la Ukambani walinde misitu , kupanda miti na kutochoma makaa.