• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 6:50 AM
Uvuvi karibu na Somalia wapigwa marufuku

Uvuvi karibu na Somalia wapigwa marufuku

NA KALUME KAZUNGU

SERIKALI imewapiga marufuku wavuvi wa Lamu na Pwani kutekeleza shughuli zao za uvuvi kwenye mpaka wa Kenya na Somalia.

Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Joseph Kanyiri, anasema ni hatia kwa wavuvi kupatikana wakitekeleza uvuvi wao kwenye eneo la Ras Kiamboni na sehemu zote za Bahari Hindi zinazopita mji wa Kiunga.

Maeneo hayo yamekaribiana na nchi jirani ya Somalia ambayo imekuwa ikishuhudia misukosuko inayochangiwa na kundi la kigaidi la Al-Shabaab.

Bw Kanyiri alisema mvuvi yeyote atakayepatikana akiendeleza shughuli zake kwenye maeneo yaliyotajwa atakuwa na kesi ya kujibu. Alisema marufuku hiyo ni kwa sababu za kiusalama.

Kulingana na ripoti kutoka kwa idara ya usalama kaunti ya Lamu, biashara bandia zimekuwa zikitekelezwa kisiri kwenye maeneo ya mpakani, hasa Ras Kiamboni.

Biashara hizo ni pamoja na ulanguzi wa binadamu, dawa za kulevya na pia bidhaa bandia.

Mvuvi wa samaki aina ya kaa, Bw Jumaa Mfariji akionyesha kaa wake aliyekuwa amevua kutoka kwa Bahari Hindi eneo la Faza. Bw Mfariji amekuwa kwenye shughuli za uvuvi kwa zaidi ya miaka 15. Picha/ Kalume Kazungu

“Ni marufuku kwa wavuvi kuendeleza shughuli zao za uvuvi kwenye Bahari Hindi, hasa zinazokaribiana na mpaka wa Kenya na Somalia. Hakuna mvuvi ataruhusiwa kuvua samaki eneo la Ras Kiamboni au kupita mji wa Kiunga ulioko Lamu Mashariki. Ukipatikana huko utakuwa na kesi ya kujibu,” akasema Bw Kanyiri.

Akigusia kuhusu marufuku ya kuvua usiku baharini, Bw Kanyiri alishikilia kuwa marufuku iliyokuwepo kwa zaidi ya miaka minane kwa sasa imeondolewa na serikali.

Aidha alishikilia kuwa lazima wavuvi watekeleze uvuvi wa usiku na mchana kwenye maeneo yanayoruhusiwa pekee na wala si sehemu zinazopakana na Somalia.

Kamishna huyo aidha alisema usajili wa wavuvi wa Lamu kwa njia ya kielektroniki unaendelea vyema kwa sasa.

Usajili huo uliamrishwa na Waziri wa Usalama wa Ndani, Fred Matiang’i mnamo Machi mwaka huu muda mfupi baada ya kuondoa marufuku ya kuvua usiku iliyodumu Lamu kwa zaidi ya miaka minane.

Marufuku ya wavuvi wa Lamu kutovua usiku ilikuwa imeamriwa na serikali ya kitaifa tangu mwaka 2011 kufuatia msururu wa uvamizi na utekaji nyara wa wavuvi na watalii baharini uliokuwa ukiendelezwa na maharamia kutoka nchini Somalia.

You can share this post!

Ruto aahidi wakazi wa Mwiki shule mpya

‘Aliyemzika’ Dedan Kimathi asimulia shujaa...

adminleo